Rais wa Ghana akiapishwa
Chama kikuu cha upinzani nchini Ghana, kimesusia sherehe za
kuapishwa kwa rais John Mahama kufuatia uchaguzi wa mwezi uliopita uliokumba na
utata.
Chama cha New Patriotic Party (NPP) kimedai Bwana Mahama alishinda uchaguzi
huo kwa njia ya udanganyifu.
Matokeo rasmi yalimpa Bwana mahama ushindi wa asilimia 50.7, ya kura zaote
zilizopigwa, kiwango ambacho kinamfanya kueouka duru ya pili ya uchaguzi dhidi
ya mgombea wa chama cha NPP Nana Akufo-Addo, ambaye alipata 47.7%.
Kabla ya kuapishwa kwake rais Mahama alitoa wito kwa rais wa nchi hiyo kuwa
watulivu na kuwa na umoja, ili kudumisha demokrasia yao ambayo kwa sasa
inakisiwa ndiyo thabiti zaidi barani Afrika.
Bwana Mahama alikuwa makamu wa rais hadi kifo cha ghafla cha rais John Atta
Mills mwezi Julai mwaka uliopita.
Kiongozi wa chama cha NPP
Tangu wakati huo amekuwa akihudumu kama kaimu rais wa nchi hiyo.
Katika hotuba yake, rais Mahama aliwaambia raia wa nchi hiyo kuwa hatapuuza
maslahi yao na kuwa atafanya kila juhudi ili kuleta maendeleo.
''Ahadi nilizotoa, ndizo ahadi nitakazo timiza'' Alisema rais Mahama.
Siku ya Ijumaa wiki iliyopita rais huyo alitoa wito kwa wabunge wa nchi hiyo
kushirikiana.
Maelfu ya wafuasi wa rais huyo walifurika bustani ya uhuru iliyko katika mji
mkuu wa nchi hiyo, Accra, kuhudhuria sherehe hiyo.
Marais kadhaa wa mataifa ya Kiafrika walihudhuria sherehe hiyo ikiwa ni
pamoja na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na rais wa Nigeria Goodluck
Jonathan.
Aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Kufuor pia alihudhuria sherehe hizo na
kukiuka matakwa na wito wa chama chake.
Kituo kimoja cha Radio cha kibinafsi nchini humo kiliripoti kuwa takriban
wafuasi 40 wa chama cha NPP walikuwa wamepiga kambi nje ya makaazi rasmi ya rais
huyo wa zamani ili kumzuia kuhudhuria sherehe hizo.
EmoticonEmoticon