Aliyejifanya mkuu wa polisi azirai kizimbani


MWANAFUNZI aliyejifanya Inspekta Mkuu wa Polisi Jumatatu alizirai mahakamani alipoamriwa alipe dhamana ya Sh500,000.
Mwanafunzi huyo, Jackson Sila Siro, mwenye umri wa miaka 20, alianguka mahakamani alipoashiriwa na ofisa wa polisi akae baada ya kuelezwa hayo na hakimu mwandamizi, Lucy Mbugua.
Siro ambaye yuko katika mwaka wa kwanza katika chuo kimoja cha teknolojia alijikuta taabani baada ya kusimamishwa kizimbani, kwa kosa la kujifanya ofisa wa polisi anayefahamika kwa jina la David Mwole Kimaiyo.
“Mshtakiwa anatoka katika familia ambayo haina mapato makubwa. Naomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana anayoweza kulipa pasipo na matatizo,” alieleza wakili wa mshtakiwa huyo. Alipewa dhamana ya pesa taslimu Sh500,000. Mshtakiwa aliashiriwa na mmoja wa maofisa wa polisi wanaomlinda atoke kizimbani.
Baada ya kutoka katika kizimba cha mahakama hiyo, mshtakiwa alitembea kwa mwendo wa pole pole kutoka kizimbani huku akitokwa na jasho.
“Mwinue tafadhali mwinue.Mwinue akae. Mtoeni nje mahala palipo na hewa,” ofisa wa polisi aliamuru baada ya mtuhumiwa huyo kudondoka na kuzirai.
“Ameanguka tu na kuzirai.Miguu yake haina nguvu,” ofisa wa polisi alieleza baada ya hakimu kuuliza kuhusu masahibu yaliyompata mtuhumiwa huyo.
Maofisa wengine wa polisi walijaribu kumwinua kutoka sakafuni lakini wakashindwa. Walimburuta kumtoa nje. Kwenye veranda mshtakiwa alitokwa na jasho kisha akaanza kulia.
“Nyamaza, Kimaiyo halii ovyoovyo. Simama si ulijifanya wewe ni Inspekta Jenerali wa polisi. Wacha kulialia. Kimaiyo anapambana kama ofisa,” mshtakiwa alifokewa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya mkasa huo wa kutaka kujipatia fedha isivyo halali ambapo alieleza kwamba alilazimika kufanya hivyo kama njia ya kumsaidia ili kupata fedha kw ajili ya kutatua matatizo yake yaliyokuw ayakimkabili chuoni.

Previous
Next Post »