Daktari mmoja aitwaye Mackod, alipitia makala
nyingi za afya ili kuweza kutambua visababishi vya vifo
ambayo havitokani na umri au nasaba ya
kiasili (genetic), na akagundua mambo tisa ambayo yanasabisha vifo ambavyo
vingeweza kuzuilika. Mambo hayo tisa ni; uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe,
ukosefu wa mazoezi, lishe duni, wadudu kama bakteria na virusi, ajali, tabia za
ngono za kupita kiasi bila kinga, vita na madawa ya kulevya.
Katika makala hii ningependa kuzungumzia
juu ya ufanyaji wa wazoezi na hasa wakati bora wa kufanya mazoezi. Mazoezi ni
muhimu sana kwa ajili ya kupunguza mafuta ya ziada mwilini, tafiti zinaonesha
kuwa asiyefanya mazoezi, madhara anayopata ni sawa na mtu anayevuta tumbaku.
Utafiti uliofanywa na Dr. Jason na Nor
Farah (2004) wa Chuo kikuu cha Glasgow, umeonesha kuwa unapofanya mazoezi kabla
ya kifungua kinywa, wakati tumbo likiwa tupu, ni bora zaidi kuliko unapoweza
kufanya mazoezi baada ya mlo wowote. Kufanya mazoezi ni jambo la maana kwa afya
kuliko kutokufanya mazoezi ya mwili, lakini unaweza kupata faida zaidi kama
unaweza kufanya kabla hujala chochote.
Mazoezi kwa ujumla wake yana umuhimu
mkubwa kwa afya ya binadamu, hasa kama yakiambatana na lishe bora. Mazoezi
huweza kuzuia magonjwa sugu kama kisukari, magonjwa ya moyo, kansa na shinikizo
la damu, pia kwa kufanya mazoezi unaweza kuongeza kipato kwa kuwa unaweza
kufanya kazi muda mrefu kuliko asiye fanya mazoezi. Familia ambazo hufanya
mazoezi huwa na afya bora na kipato kikubwa kwa kuwa fedha kidogo wanazopata
hutumika kwenye maendeleo ambapo familia wasiofanya mazoezi, hujikuta wakitumia
kipato hicho kidogo kwa ajili ya magonjwa ambayo yangeepukika kwa kufanya
mazoezi.
Pia kwa kufanya mazoezi kila mara na hasa
kabla ya mlo kuna faida nyingi ambazo haziwezi kuonekana kwa haraka, kama vile
kuimarisha hali ya kiakili, ambayo matokeo yake ni kuwa na furaha. Hii
inatokana na kuzalishwa kwa wingi kwa kemikali aina ya endorphins wakati wa
kufanya mazoezi. Kemikali hii ya endorphins ni muhimu kwenye mapambano ya
sonono (depression) na hivyo kumfanya mfanya mazoezi kuwa na furaha zaidi.
Tafiti zinaonesha kuwa mwili huzalisha kemikali hii ya endorphins baada ya mtu
kufanya mazoezi ya kawaida kwa dakika 12. Kama wanafamilia wanaweza kufanya
mazoezi kwa muda hata wa saa moja, au nusu saa, wanaweza kuwa na furaha na
kuzuia kusambaratika kwa ndoa zao.
Ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara husaidia
pia mfanya mazoezi ajithamini, na kuondoa uchovu na unyonge. Unapojithamini,
pia inaleta tokeo ya kujiona bora na kuwa mwenye ustawi. Mazoezi pia hufanya
tendo la ndoa kuwa bora na hivyo kuleta mahusiano bora ya kinyumba na mpwendwa
wako.
Nimejaribu kuanisha umuhimu na faida za
maozezi na hasa wakati yanapokuwa na tija ili kuleta hamasa ya kufanya mazoezi
kwa kila msomaji wa makala hii. Unaweza kufanya mazoezi wewe na familia yako au
na wenzako, au pekee yako, chukua muda kidogo katika masaa 24 na ufanye
mazoezi, maana utajisikia vizuri na kuwa mwenye afya, lakini kumbuka utapata
faida zaidi ukifanya mazoezi wakati tumbo likiwa tupu, yaani kabla ya mlo,
baada ya kula chakula tembea taratibu ili kukifanya kitulie vema tumboni.
Usisahau, kabla ya kifungua kinywa asubuhi
jitahidi ufanye mazoezi angalau kwa muda wa robo saa.
EmoticonEmoticon