Mkuu
wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko Olivary Kamili akiagalia
wanafunzi wakijipanga tayari kuingia madarasani kuanza masomo.(Picha na
Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Kaimu
Mratibu Elimu kata ya Ikungi wilayani Ikungi Mwalimu Olivary Kamilly,
amewaagiza walimu wa shule za msingi katika kata hiyo, kuhakikisha
wanadahili watoto wote walemavu wenye sifa za kuanza darasa la kwanza
mwakani.
Mwalimu
Kamillya amesema zoezi hilo la kudahili watoto walemavu litakalofanyika
mwezi wa 12 mwaka huu, liende sambamba na kudahili watoto wasio na
ulemavu wenye sifa ya kuanza darasa la kwanza mwakani.
Amesema
uzoefu unaonyesha wazi kwamba watoto wengi walemavu wa umri wa kwenda
shule, wamekuwa wakikosa fursa ya kupata haki yao ya msingi ya kupata
elimu kutokana na sababu mbalimbali.
Aidha,
amesema kuwa kutowadahili watoto wenye ulemavu kipindi cha Disemba kila
mwaka, kunasababisha watoto hao kuanza masomo katika shule za msingi
wakiwa na umri mkubwa.
Mwalimu
Kamilly ambaye pia ni mwalimu mkuu shule ya msingi mchanganyiko Ikungi,
ametaja baadhi ya sababu zinazochangia watoto hao kukosa elimu ni
pamoja na ukosefu wa miundo mbinu rafiki na upungufu wa shule ambazo
zina uwezo wa kudahili watoto walemavu.
Amesema pamoja na changamoto hizo, atahakikisha shule za msingi
zilizopo kwenye kata yake, zinakuwa na uwezo wa kudahili watoto wenye
ulemavu kwa asilimia 90 au wote waliopo kwenye kata yake.
Katika
hatua nyingine, Mwalimu Kamilly ameiomba serikali kuangalia uwezekano
wa kuboresha mfumo wa utoaji wa elimu katika vyuo vya ualimu kwa
kuongeza elimu maalum, ili kila mwalimu anayehitimu awe na elimu
inayojumuisha pia elimu maalum.
Akifafanua
amesema elimu maalum itakayomsaidia kila mwalimu atakapoingia katika
kazi ya ufundishaji, aweze kufundisha kwa ufasaha watoto wote wenye
ulemavu na wasio na ulemavu.
EmoticonEmoticon