Waziri wa sheria wa Afrika Kusini ametaka ufafanuzi
zaidi kuhusu wachimba migodi 270, walioshtakiwa kwa kosa la mauaji ya
wachimba migodi wenzao waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Waziri Jeff Radebe alisema kuwa uamuzi wa
kuwafungulia mashtaka wachimba migodi hao, uliwashtua wengi na
kusababisha wasiwasi miongoni mwa watu nchini humo.
Inaarifiwa
viongozi wa mashtaka waliwafungulia mashtaka wachimba migodi hao kwa
misingi ya kanuni za kosa la kutendwa kwa nia moja ambayo ilitumika sana
wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi.
Uamuzi huo tayari umekashifiwa vikali na mawakili ya kikatiba.
Katika taarifa yake, waziri Radebe, alisema kuwa
kulingana na katiba , waziri wa sheria ndiye ana usemi mkubwa juu ya
mamlaka ya kitaifa kuhusu mashtaka.
Alisema kuwa ameagiza kiongozi wa mamlaka hiyo kumpa maelezo kuhusu sababu za uamuzi waliouchukua.
Polisi waliwapiga risasi wachimba migodi 34 wiki
mbili zilizopita wakati wa mgomo wao katika mgodi wa madini ya Paltinum
wa Marikana , unaomilikiwa na kampuni ya Lonmin, ambayo ni ya tatu kwa
ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo.
Mgomo wa wachimba migodi
Watu wengi walighadhabishwa na mauaji hayo.
Hata hivyo polisi walitetea hatua yao wakisema
walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao, walipokuwa
wanakabiliana nao wakiwa wamejihami kwa mapanga.
Sita kati ya wachimba migodi hao 270 waliokamatwa na polisi wangali hospitalini wakiuguza majeraha yao.
Walifunguliwa mashtaka siku ya Alhamisi baada ya
viongozi wa mashtaka kusema kuwa walikuwa miongoni mwa kundi la watu
ambao vitendo vyao vilisababisha polisi kuwafyatulia risasi.
EmoticonEmoticon