MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka mikakati mitano ya kuboresha
ukusanyaji kodi ya majengo, ikiwamo kutathmini majengo ili kupanga
viwango rafiki vya kodi kwa walipakodi.
Mikakati mingine ni kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa ukusanyaji,
kutoa elimu kwa jamii kuhusu ulipaji kodi, kushughulikia pingamizi za
kodi kwa wakati na kuboresha orodha ya uthamini ili kuwa na takwimu
sahihi.
Ofisa Msaidizi wa Huduma ya Mlipakodi ya TRA, Maya Magimba alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu umuhimu
wa kodi.
Alisema kodi ni muhimu kwa Serikali kwa vile inatumika kuendesha
shughuli za kijamii, ukiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, zahanati
na madarasa.
“Tutahakikisha nyaraka za usajili zinatunzwa na mlipakodi kwa kufuata taratibu ili kuepuka usumbufu,” alisema.
Alisema kodi ya majengo hulipwa kuanzia Januari mosi hadi Machi 31 kila
mwaka bila adhabu, na baada ya Aprili mosi hulipwa na adhabu, kodi ya
pango la ardhi hulipwa kuanzia Julai mosi hadi Desemba 31 kila mwaka.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Mboza Maige alisema mwananchi au
taasisi yenye nyaraka za umiliki wa ardhi ya Serikali anapaswa kulipa
kodi hiyo.
Alisema iwapo eneo litakuwa na maendelezo ya jengo la kudumu na linatumika, mtu huyo atalazimika kulipa kodi mbili.
EmoticonEmoticon