Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kuwa serikali yake itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda vipya ili kufanikisha nia yake ya kuzalisha ajira nyingi, kukuza uchumi na kuiwezesha serikali kukusanya mapato zaidi.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 31 Mei, 2016 katika hafla ya kutoa tuzo ya Rais kwa wazalishaji bora wa mwaka 2015, iliyofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam.
Dkt. Magufuli amesema serikali yake inatambua umuhimu wa viwanda katika uchumi na amewataka wenye viwanda na wenye nia ya kuanzisha viwanda kupuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wanaodai anawachukia wenye viwanda.
“Wekezeni kwenye viwanda na mimi nawaambia mkishindwa katika kipindi hiki cha awamu ya tano, hamtaweza tena.
“Mimi siwachukii wenye viwanda na wala siwachukii matajiri” Amesema Rais Magufuli huku akisisitiza kuwa serikali yake itafanyia kazi changamoto zilizotolewa na wenye viwanda zikiwemo miundombinu duni ya usafirishaji, nishati, mikopo na kodi.
Rais Magufuli pia ametoa wito kwa benki zinazoendesha shughuli zake hapa nchini kujenga mazingira bora kwa wanaohitaji mikopo kwa ajili ya kuanzisha viwanda ikiwemo kupunguza riba na amebainisha kuwa pamoja na kuimarisha benki ya uwekezaji (TIB), serikali yake pia inakusudia kuanzisha benki ya viwanda ili kuharakisha uanzishaji wa viwanda.
Amewahakikishia wenye viwanda kuwa serikali yake itavilinda viwanda vya ndani na kutaka wafanyabiashara wengi zaidi wajielekeza kuanzisha viwanda, badala ya kuendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi licha ya malighafi nyingi kuwepo hapahapa nchini.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli ametoa tuzo kwa washindi mbalimbali wa uzalishaji bora wa bidha za viwandani ambapo kampuni ya bia ya TBL imeibuka mshindi wa jumla.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
31 Mei, 2016
EmoticonEmoticon