Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally
Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo
wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza mapato
ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Rais Magufuli amechukua hatua
hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kufanya
kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Tarehe 22 Machi, 2013
Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya
uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo
ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza
kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za
ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa
kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na kuivunja bodi ya
TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu
wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.
Aidha, Rais Magufuli amewataka
Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua
hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani
(Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
“Waziri hakikisha unachukua
hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na
sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote
atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar
es salaam
26
Aprili, 2016
EmoticonEmoticon