Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka watendaji
wa Shirika la Reli nchini (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli
(RAHCO) kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani
Kilosa mkoani Morogoro inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za
treni kurejea.
Prof.
Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa
hadi Magulu- Kidete kuona athari zilizosababishwa na mafuriko
yaliotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma.
“ Fanyeni
kazi usiku na mchana ili ikifika alhamisi mawasiliano ya reli kati ya
mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata
huduma ya treni ,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewahakikishia
wananchi wa vijiji vya Munisagara,Mkadage,Mzaganza ,Magulu na Kidete
ambao usafiri wao pekee wa uhakiki ni wa kutumia reli watoe ushirikiano
kwa serikali ili ukarabati na ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka.
Amewataka
wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa kupanda
miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi
wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
“Pandeni
miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya uharibifu wa
mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe
kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” amesisitiza Waziri Prof.
Mbarawa.
Naye
Diwani wa kata ya Kidete Bw. Mohamed Seleman Mbunda amemhakikishia
Waziri Mbarawa kuwa wananchi wake watashirikiana na serikali kulinda
mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila
wakati wilayani humo.
Mafuriko
wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa
na Dodoma ambayo husababisha maji ya mto mkondoa kuacha mkondo wake na
kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati.
Mvua za
hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma zimesomba reli katika
eneo la Magulu—Kidete kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata
mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa.
Katika
hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa TRL na RAHCO
kutafuta suluhisho la kudumu katika madaraja 32 yaliokatika mtandao wa
reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.
EmoticonEmoticon