Mgombea
urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad amesema kama atapewa ridhaa ya kuwa rais atahakikisha
Zanzibar inapata mamlaka kamili.
Akihutubia
wananchi leo kwenye uzinduzi wa kampeni za Cuf katika viwanja vya
Kibanda Maiti visiwani Zanzibar, Maalim Seif amesema kuwa kama wananchi
watamchagua atapigania kupata serikali ya Muungano yenye serikali tatu.
“Kama
mtanichagua kitu cha kwanza, nawaahidi wananchi wa Zanzibar ni kupata
serikali ya muungano yenye serikali tatu… Zanzibar kuwa na mamlaka
kamili na kurejesha rasimu ya Jaji Warioba’’ amesema Maalim.
Hii ni mara ya tano kwa Maalim ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kugombea nafasi ya urais.
Mgombea
huyo ambaye ametumia dakika zisizozidi 15 kueleza vipaumbele vya
serikali yake, amesema kuwa atarejesha misingi ya utawala bora ili
wananchi waishi kwa amani.
Pia
Maalim ameeleza kuwa, atahakikisha anajenga uchumi imara na unaokua kwa
kasi ikiwa ni sehemu ya ndoto yake ya siku nyingi katika harakati za
maendeleo.
“lingine
ni kujenga uchumi imara na unaokuwa kwa kasi, hiyo ndio ndoto yangu ya
kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki… kwa kuhakikisha
kujenga bandari ya kisasa, sio kwa maneno lakini kwa matendo’’ alisema.
Sambamba
na hayo, amewaahidi vijana kupata ajira na mitaji ili kujiendeleza
kimaisha ‘’ Nitafungua benki ya uwekezaji ya Zanzibar ili kutoa mitaji
kwa vijana wetu wanaojihusisha na uvuvi ili wamudu kujiendeleza na
kujiajiri’’ alisisitiza Maalim.
Aidha,
katika kumalizia vipaumbele vyake, Maalim ameahidi kuwa siku 100 za
mwanzo ndani ya utawala wake atahakikisha sheria ya mafuta na gesi
inapatikana ili kuanza kuchimba mafuta visiwani humo.
Katika
uzinduzi huo wa kampeni, pamoja na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi,
viongozi mbalimbali, pia tukio hilo limehudhuriwa na mgombea urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa
Ukawa, Edward Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Haji.
EmoticonEmoticon