JUMLA ya
watahiniwa 775,729 wanatarajiwa kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi utakaofanyika leo na kesho nchi mzima. Aidha, serikali imesema
hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kumzuia mtahiniwa yeyote kufanya
mtihani kwa sababu yoyote ile, hata ikiwa ni kutolipa ada.
Akizungumza
jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk Charles
Msonde alisema kati ya hao, watahiniwa wavulana ni 361,502 ambao ni sawa
na asilimia 46.6 na wasichana ni 414,227 sawa na asilimia 53.4.
Watahiniwa
wasioona walioandikishwa kufanya mtihani ni 76, wakiwemo wavulana 49 na
wasichana 27 wakati wale wenye uoni hafifu wanaohitaji maandishi
makubwa ni 698, wavulana wakiwa ni 330 na wasichana 368.
“Watahiniwa
748,514 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 27,215
watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia
katika kujifunzia,” alisema. Msonde alisema katika siku mbili za
mtihani, watahiniwa watatahiniwa kwa masomo ya Kiswahili, Kiingereza,
Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Aidha,
Msonde aliwaasa wanafunzi, walimu na wananchi kutojihusisha na vitendo
vya udanganyifu wa mtihani na kuwa Baraza halitasita kumchukulia hatua
yeyote atakayeshiriki kwenye udanganifu, ikiwa ni pamoja na kuwafutia
matokeo yote watahiniwa watakaobainika kujihusisha na vitendo ya
udanganyifu.
Msonde
alitoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na wilaya, kuhakikisha
taratibu za mitihani zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
mazingira ya vituo ni salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu.
Kwa
upande wa wasimamizi, Msonde aliwataka kufanya kazi kwa umakini na
uadilifu na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, kwani Baraza
halitasita kuchukua hatua yoyote dhidi ya atakayebainika kukiuka
taratibu za uendeshaji wa mtihani wa Taifa.
Kuhusu
kuwazuia watahiniwa kufanya mtihani kwa kisingizio cha kutolipa ada,
Msonde alisema mtihani wa darasa la saba ni bure na hauna uhusiano na
mwanafunzi kutolipa ada au sababu zingine.
“Hakuna
mtu yeyote ambaye anaruhusiwa kumzuia mtahiniwa ambaye amejiandikisha
kufanya mtihani mwaka huu, hivyo wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao
wanakwenda kwenye vituo vya mitihani,” alisema.
EmoticonEmoticon