WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la
uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili
kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.
Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa
Katoliki cha Kibaoni wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri
Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia
Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa
yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo la Katavi.
Amesema yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na
kwa vile atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika
mikakati mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze
kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Mheshimiwa Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika
kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu
wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao.
Akimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani
Mlele, Padri Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele
kumuenzi Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa
amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea
maendeleo.
Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.
Leo saa 10 jioni ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 19, 2015.
EmoticonEmoticon