Anayedaiwa kukata nyeti za mume Nyeri ashtakiwa


Bi Valentine Mugure
Bi Valentine Mugure akiwa mahakamani Nyeri Juni 10, 2015. Picha/JOSEPH KANYI  

Valentine Mugure anayedaiwa kukata sehemu nyeti za mpenziwe mjini Nyeri amefikishwa kortini na kukanusha mashtaka. Amewekwa rumande uchunguzi ukiendelea.

MWANAMKE anayedaiwa kukata sehemu nyeti za mpenziwe mjini Nyeri amefikishwa kortini na kushtakiwa kumshambulia na kumdhulumu mwanamume huyo.
Valentine Mugure, 25 aliwasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi J Aringo.
Alidaiwa kumshambulia Bw Paul Mwangi, 26, mhasibu wa Maathai Supermarket, na kumkata kwa kisu begani na sehemu nyeti Jumanne asubuhi eneo la Gamerock karibu na mji wa Nyeri kufuatia mzozo wa kinyumbani unaoaminika kuwa ulihusu pesa. Polisi walimtia mbaroni muda mfupi baadaye.
Mshtakiwa alikanusha mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani na polisi.
Upande wa mashtaka uliwasilisha ombi kuwa mshtakiwa awekwe rumande maanake mwathirika bado amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nyeri katika hali mbaya baada ya kufanyiwa upasuaji.
Hakimu Mkazi Aringo aliamua Mugure awekwe rumande akisubiri kutajwa kwa kesi hiyo Juni 15 mwezi huu.
Previous
Next Post »