TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 20.05.2015.






·         MTU MMOJA JINSI YA KIUME AMEUAWA KWA KUPIGWA NA WANANCHI KUTOKANA NA TUHUMA ZA WIZI JIJINI MBEYA.

·         MTEMBEA KWA MIGUU AFARIKI DUNIA PAPO HAPO BAADA YA KUGONGWA NA GARI.

·         WATU WATATU WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA WAKIWA WAMEPANDA MICHE 200 YA BHANGI HUKU WAKIWA NA BHANGI DEBE MOJA.

KATIKA TUKIO LA KWANZA:

MTU MMOJA AMBAYE HAKUWEZA KUFAHAMIKA JINA LAKE MARA MOJA, JINSI YA KIUME MWENYE UMRI KATI YA MIAKA 25-30, ALIUAWA KWA KUPIGWA NA KUNDI LA WANANCHI WALIOAMUA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI NA KISHA KUCHOMWA MOTO.

TUKIO HILO LIMETOKEA USIKU WA KUAMKIA LEO MAJIRA YA SAA 03:30 HUKO KATIKA ENEO LA ISENGO-AIRPORT, KATA YA IYELA, TARAFA YA IYUNGA, JIJI NA MKOA WA MBEYA.

INADAIWA KUWA CHANZO CHA KIFO CHAKE NI KUTOKA DAMU NYINGI BAADA YA KUPIGWA NA WANANCHI KUTOKANA NA TUHUMA ZA WIZI. MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA HOSPITALI YA RUFAA MBEYA.

KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI NYIGESA R. WANKYO ANATOA WITO KWA WANANCHI KUACHA TABIA YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI NA BADALA YAKE WAJENGE TABIA YA KUWAFIKISHA KATIKA MAMLAKA HUSIKA WATUHUMIWA WANAOWAKAMATA KWA TUHUMA MBALIMBALI KWA HATUA ZAIDI ZA KISHERIA.



KATIKA TUKIO LA PILI:

MTEMBEA KWA MIGUU MMOJA ALIYEFAHAMIKA KWA JINA LA ANESTA ADAM @ MPEMBA (67) MKAZI WA KIJIJI CHA KALOLENI - SONGWE ALIFARIKI DUNIA PAPO HAPO BAADA YA KUGONGWA NA GARI LENYE NAMBA ZA USAJILI T.948 AFM AINA YA FUSO IKIENDESHWA NA DEREVA ASIYEFAHAMIKA JINA WALA MAKAZI YAKE IKIWA INAVUTA GARI NYINGINE T.160 AAX AINA YA M/FUSO.

TUKIO HILO LIMETOKEA MNAMO TAREHE 19.05.2015 MAJIRA YA SAA 20:05 USIKU HUKO ENEO LA SONGWE MAGOROFANI, KATA YA SONGWE, TARAFA USONGWE, WILAYA YA MBEYA VIJIJINI, MKOA WA MBEYA KATIKA BARABARA KUU YA MBEYA/TUNDUMA.

AIDHA KATIKA AJALI HIYO, GARI NYINGINE NDOGO YENYE NAMBA ZA USAJILI T.226 ANQ AINA YA TOYOTA COROLLA ILIYOKUWA IMEPAKI PEMBENI YA BARABARA ILIGONGWA NA MAGARI HAYO YALIYOKUWA YAKIVUTANA NA KUSABABISHA UHALIBIFU WA GARI HIYO. CHANZO CHA AJALI KINACHUNGUZWA. DEREVA ALIKIMBIA MARA BAADA YA TUKIO NA JUHUDI ZA KUMTAFUTA ZINAENDELEA.


TAARIFA ZA MISAKO:

JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATU WATATU WALIOFAHAMIKA KWA MAJINA YA 1. DAVID JAPHET (38) 2. BONIFACE JACKSON (28) NA 3. DANIEL SHADRACK (20) WOTE WAKAZI WA KONDE WILAYANI CHUNYA WAKIWA WAMEPANDA BHANGI MICHE  200 PAMOJA NA BHANGI DEBE MOJA SAWA NA UZITO WA KILO 6.

WATUHUMIWA HAO WALIKAMATWA KATIKA MSAKO ULIOFANYIKA MNAMO TAREHE 19.05.2015 MAJIRA YA SAA 10:30 ASUBUHI HUKO KATIKA KITONGOJI CHA KONDE, KIJIJI NA KATA YA MATWEGO, TARAFA YA KIPEMBAWE, WILAYA YA CHUNYA, MKOA WA MBEYA. 

KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI NYIGESA R. WANKYO ANATOA WITO KWA JAMII KUACHA KUJIHUSISHA NA BIASHARA HARAMU YA BHANGI KWANI NI KINYUME CHA SHERIA. AIDHA ANATOA WITO KWA JAMII KUTOA TAARIFA KATIKA MAMLAKA HUSIKA ZA MTU/WATU WANAOJIHUSISHA NA ULIMAJI WA ZAO HARAMU LA BHANGI ILI WAKAMATWE NA HATUA ZA KISHERIA ZICHUKULIWE DHIDI YAO.


Imesainiwa na:
[NYIGESA R. WANKYO – ACP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
Previous
Next Post »