
·
Ni kweli ngazi ya vyama tawala na mikutano ya upatanishi
kufanyika Arusha.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa Tanzania
imekubali kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa ndani ya chama tawala cha Sudan
Kusini cha Sudanese People’s Liberation
Movement (SPLM), mgogoro ambao umesababisha kuzuka kwa vita ya wenyewe
kwa wenyewe nchini humo.
Hata hivyo, Rais Kikwete
amesema kuwa usuluhishi huo utakuwa wa kichama na Chama cha Mapinduzi (CCM)
ndicho kitaongoza usuluhishi huo katika mazungumzo yatakayofanyika Arusha na
kuwa jitihada hizo za Tanzania hazitaingilia mazungumzo ya kujaribu kusimamisha
mapigano nchini humo yanayoendelea huko Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Kikwete amesema
kuwa ulikuwa uongozi wa SPLM na hasa Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Salva Kiir
ambao wameiomba Tanzania kusaidia jitihada za kisiasa za kupatanisha pande
ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya SPLM wakiamini kuwa mapatano ndani
ya chama yatafanikisha kumaliza mgogoro wa kisiasa katika Serikali ya nchi hiyo
ambayo imegawanyika na kusababisha vita
vya wenyewe kwa wenyewe.
Rais Kikwete ametangaza
jitihada hizo za upatanishi za Tanzania wakati alipohutubia maelfu kwa maelfu
ya wananchi na kupitia kwao Taifa kwenye Sherehe ya Kuzima Mwenge wa Uhuru,
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Kilele cha Wiki ya Vijana kwenye Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Rais Kikwete amewaambia
wananchi kuwa Tanzania imekubali kuwasaidia ndugu zao wa Sudan Kusini kwa nia
ya kutimiza wajibu wake wa kimataifa na kwa kuongozwa na kaulimbiu ya Oktoba
Mwaka 1959 ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliitoa wakati nchi ya
Tanganyika bado ikidai uhuru wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza.
Rais Kikwete ameikariri
kaulimbiu hiyo maarufu: “Sisi Watu wa Tanganyika tunataka kuwasha
Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka yetu,
ulete tumaini pale ambako hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na
heshima palipojaa dharau.”
Rais Kikwete amesema
kuwa Mwenge wa Uhuru unabeba falsafa kubwa ndani yake kuhusu “nchi
yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge, wenye dhiki na
wasiokuwa na amani. Dhamira hii ya Mwalimu na nchi yetu ilitimizwa Desemba 9,
1961, siku Tanganyika ilipopata Uhuru ambako Bendera ya Taifa huru la
Tanganyika na Mwenge wa Uhuru vilipandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro
na Mwenge kuwashwa.”
“Toka wakati huo mpaka
sasa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima ukipita katika mitaa,
vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja,
upendo, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Kwa kuzingatia ujumbe uliobebwa na Mwenge wa
Uhuru, nchi yetu na sisi Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu
zetu Barani Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya
wakoloni na wabaguzi wa rangi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni fahari kwetu kwamba
wananchi wa Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini nao wako huru
na tumetoa mchango wetu. Ni jambo la
faraja kubwa kwamba nchi yetu imeweza kupatia hifadhi ndugu zetu wa nchi jirani
na hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya kukosekana
kwa amani ama kukimbia mateso ya uongozi wa kidikteta. Ndugu zetu wa Kongo,
Burundi, Rwanda, Kenya na Comoro wanaujua ukweli huo. Na, kwa Uganda
tuliwasaidia kuling’oa Dikteta Idd Amin na Comoro tulisaidia kuunganisha nchi
yao tena.”
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
15 Oktoba,2014
EmoticonEmoticon