Hali ya simanzi imetawala miongoni mwa wakazi wa Makete mjini mkoani Njombe kufuatia utingo wa lori lililobeba skaveta kugongwa na lori hilo hadi kufa papo hapo.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11:45 alfajiri wakati lori hilo likipita kwenye eneo lililolundikwa vifusi kufuatia matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Akizungumza na eddy blog mkuu wa polisi wilaya ya Makete Bw. Alfred Kasonde amemtaja marehemu kuwa ni Albert Mwalukasa (21) ambaye amegongwa na lori hilo lenye namba za usajili T 489 BDW mali ya Timoth Mwalukasa mkazi wa mkoa wa Mbeya.
Lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Bw. Lewad Mekule ambaye kwa sasa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano zaidi na upelelezi tayari umekamilika hivyo atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji yanayomkabili.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia Maiti cha hospitali ya wilaya ya Makete ukisubiri ndugu wa marehemu waliopo mkoani Mbeya kufika kuuchukua kwa ajili ya taratibu za kumzika.
Baba mdogo wa marehemu aitwaye Allan Mwalukasa ambaye alikuwepo kwenye lori hilo amesema hata yeye anashangaa kilichopelekea kifo cha ndugu yake kimetokeaje.
"Nilikuwa mbele hapa naangalia sehemu ambayo kidogo ni nzuri kwa ajili ya vifusi hapa ambavyo vimelundikwa barabarani ghafla nkashangaa nimesikia kelele nyuma huko analia aaaaah nikashindwa kuelewa, kuja kukimbia ninamkuta yupo chini ya gari, huyo ni mtoto wa kaka yangu ambaye tumefuatana" amesema Mwalukasa.
Kwa upande wa wananchi waliofika eneo la tukio wamesema marehemu alikuwa akimuongoza dereva namna ya kupitisha lori kwenye vifusi vilivyolundikwa muda mrefu barabarani bila kusambazwa, lakini ghafla aliteleza kwa kuwa alikuwa akipita juu ya vifusi hivyo ndipo alipogongwa na kufariki papo hapo.
Wananchi hao wametupa lawama kutokana na vifusi hivyo kukaa muda mrefu bila kusambazwa hali inayopelekea usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo, na hivi karibuni mwandishi wetu alizungumza na mkandarasi wa ujenzi huo ambaye alisema amekwenda Morogoro kufuata vifaa vya kumalilisha ujenzi huo.
Hata hivyo wameshauri barabara mbadala zilizojengwa na mkandarasi huyo zitumike ili kuepusha madhara zaidi.
EmoticonEmoticon