Adaiwa kuiba mtoto kulinda ndoa yake

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwanamke mmoja wilayani Igunga Tabora anatuhumiwa kwa kuiba mtoto mwenye umri wa miezi minne(4),ili aweze kulinda ndoa yake isivunjike kutokana na mumewe kuhitaji mtoto kwa muda mrefu.
 Kamanda wa Polisi Tabora, Antony Lutta alithibitisha kutokea kwa wizi huo wa mtoto na kuongeza kuwa tukio hilo limetokea Februari 26, mwaka huu saa saba mchana.
Alimtaja mwanamke aliyeiba mtoto huyo kuwa ni Zawadi Jacobo mkazi wa Mtaa wa Warabuni Igunga, kuwa saa saba mchana alikwenda kwenye kibanda cha kuuzia pombe maarufu kwa jina la grocery na kuagiza kinywaji aina ya soda.
Lutta aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuagiza kinywaji hicho, mwanamke huyo aliomba mtoto kumbeba kwa mama mtoto aliyefahamika jina la Martina Joseph (21) mkazi wa Igunga huku kichanga hicho kilichoibiwa kikifahamika kwa jina la Matha Joseph miezi mine(4).
Alisema alipopewa mtoto huyo alitokomea pasipojulikana hadi alipokamatwa huko Misigiri Singinda akielekea kwa mumewe kwa lengo la kumueleza tayari kisha jifungua mtoto wa kike.
Mama wa mtoto huyo akizungumza na gazeti hili, alisema kuwa alipomkosa mwanawe alitoa taarifa polisi haraka huku jitihada za wananchi zikiendelea kufanyika ili kumtafuta mwanamke huyo.
Kamanda Lutta alisema taarifa hizo zilipo fika polisi, jeshi hilo lilianza kazi yake kwa haraka kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, hata hivyo saa tisa jioni mtoto huyo alipatikana huko Misigiri.
Alisema mwanamke huyo anashikiliwa na polisi pindi upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili dhidi ya wizi huo wa mtoto.



 
Previous
Next Post »