Serikali yatakiwa kupeleka vifaa vya kupimia Ebola mpaka wa Tanzania na Zambia mjini Tunduma.

Serikali imeombwa kupeleka haraka vifaa vyenye uwezo wa kuwatambua watu wenye maambukizi ya ugonjwa wa ebola katika mpaka wa Tanzania na Zambia mjini Tunduma ili kuepusha ugonjwa huo kuingia nchini kirahisi kupitia katika mpaka huo ambao unatumiwa na nchi zaidi ya sita za kusini mwa afrika.
Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wakazi wa mji wa Tunduma ambao wamedai kuwa hadi hivi sasa hakuna elimu waliyoipata ya kujikinga na ugonjwa wa ebola wala hatua za tahadhari ambazo zimechukuliwa na serikali dhidi ya wageni wanaoingia nchini kupitia mpaka huo.
 
 mpaka huo wenye pilikapilika nyingi na kushuhudia watu wengi wakiingia na kutoka nchini kwa miguu na magari bila ya kuwepo kwa aina yoyote ya ukaguzi wa kiafya, huku kaimu afisa afya wa mpaka huo Bw. Jamal Mohamed akidai kuwa bado ofisi yake haijapata vifaa vya kufanyia ukaguzi wa kiafya kwa wageni wala watumishi wa idara ya afya hawajawezeshwa kujikinga wao wenyewe na ugonjwa wa ebola.
 
Kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa kamati ya ulinzi mipakani mkoani Mbeya ambaye pia ni kamishna msaidizi wa idara ya uhamiaji katika mpaka wa Tunduma Bw. Lusarago Mleka amesema kuwa ingawa hakuna mtu ambaye ameshagundulika kuambukizwa ugonjwa huo katika mpaka wa Tunduma bado kuna hofu kubwa kwa watumishi wa idara ya uhamiaji hasa wanapohudumia watu wanaotokea upande wa Tanzania kutokana na kutokuwepo na udhibiti wa kiafya kwa watu hao.
Previous
Next Post »