TAARIFA KWA UMMA KUTOKA KITENGO CHA VIJANA NCCR-MAGEUZI






 1.0 UONGOZI WA KITENGO CHA VIJANA
Tunapenda kuvitaarifu vyombo vya habari na umma kwa ujumla kuwa, tulikuwa na mchakato wa kuwapata viongozi wa kitengo cha vijana ambao ulianza kwa vijana kuchagua na kupendekeza viongozi waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya kitengo na baadae kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Katiba ya NCCR-Mageuzi na kanuni za vitengo vya chama, hivyo kutokana na mchakato huo, kitengo cha vijana kimepata viongozi wafuatao:

1. Ndugu Deo Meck – Mwenyekiti Kitengo cha Vijana Taifa
2. Ndugu Hassan Ruhwanya – Makamu Mwenyekiti Kitengo cha Vijana Tanzania Bara
3. Ndugu Mawazo M. Athanas – Katibu Mkuu Kitengo cha vijana Taifa.

4. Ndugu Simon Noel – Naibu Katibu Mkuu Kitengo cha Vijana Tanzania Bara
Hivyo tunaomba ushirikiano katika ukuzaji na uendelezaji wa demokrasia na uwajibikaji nchini kwa faida na maendeleo ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

2.0 KUHUSU SAKATA LA AKAUNTI YA ECROW
Tunaunga mkono harakati za chama na Mh. David Kafulila (Mbunge wa Kigoma kusini) za kutaka kuwepo na uchunguzi huru na wa haki kuhusu sakata la fedha za akaunti maalum ya IPTL, (Escrow account).

Tunataka wajue kuwa vitisho, ubaguzi, udhalilishaji, fedheha na unyanyapaa havitaweza kufifisha harakati za kuhoji na kuwawajibisha wasiowajibika.

Tunatambua kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Eliakimu Maswi, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ni sehemu ya watu muhimu katika upatikanaji wa ukweli juu ya sakati la hizi pesa, lakini cha ajabu wamekuwa wakali kama mbogo na kulifanya jambo hili binafsi badala ya kujibu hoja zilizotolewa na kuelekezwa kwenye taasisi wanazoziongoza, jambo linalotia shaka usafi wao katika hili jambo.

Ni aibu kubwa kwamba mwanasheria Mkuu wa serikali, Mtu anayepaswa kuonyesha staha, kuheshimu haki za binadamu, kutambua na kuheshimu uumbaji wa Mungu, kuheshimu utu na ubinadamu, na badala yake anaudhalilisha kwa kumuita binadamu tumbili.

Hiyo ni dharau kubwa na tusi kubwa kwa bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hata tumbili anahudhuria na kuwa sehemu ya vikao vya bunge na kuwa sehemu ya mjadala. 

Sio hivyo tu, bali ni kuwadhalilisha, kuwatukana na kuwafedhehesha wakazi na wapiga kura wa kigoma kusini kuwa wanawakilishwa na tumbili bungeni, tafsiri yake ni kuwa nao ni tumbili na wamemchagua tumbili mwenzao kuwawakilisha bungeni, tunamtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ajiudhuru au awajibishwe na Mh. Rais kwakuidhalilisha ofisi anayoitumikia na pia mamlaka na taasisi iliyomteua.

Pia tunamtaka Katibu Mkuu wa wizara ya nishati na madini, Ndugu Eliakimu Maswi aache vitisho, ubabe na ulevi wa madaraka na awajibike kwa wizi uliofanyika kupitia wizara anayoiongoza. Kama anafikiri majibu ya hoja hizo ni ngumi basi hajui dhamana na wajibu aliopewa na kuaminiwa kuwa anaweza kuubeba.

Ni aibu kubwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na madini, na hali ya kutojali kwa kiwango kikubwa utu wa Mtanzania, kutokuwa hata na chembe ya uzalendo, kudhalilisha familia zao, kudhalilisha ofisi wanazosimamia, kudhalilisha elimu na taaluma zao, kuonyesha ni jinsi gani elimu haijawasaidia kujitambua na kudhalilisha shule na vyuo walivyosoma, kudhalilisha waalimu waliowafundisha kuwa malipo ya mafunzo yote na kodi zote zilizotumika kuwaelimisha kuwa faida na majibu yake ni kufanikisha wizi wa pesa za watanzania walipa kodi, wanyonge na masikini, wanaoshindia mlo mmoja au kupitisha siku bila chakula, ambao watoto wao wanakaa chini madarasani kwa kukosa madawati, wanakosa waalimu, vitabu na elimu bora, wanaokufa kwa kukosa dawa, zahanati na huduma za matibabu.

Tunawataka wajue kuwa vitisho havina uwezo wa kufifisha harakati za kuwawajibisha, wajue kuwa hawana uwezo wa kutupiga ngumi watanzania wote, hawana uwezo wa kutukata vichwa watanzania wote, na wajue iwe kwa matusi, vitisho, fedheha watuhumiwa wakithibitishwa kukwapua pesa hizo lazima warudishe fedha za umma, kama kudai na kutetea maslahi na rasilimali za umma ni kuitwa tumbili basi tuko tayari kuitwa tumbili lakini mrudishe pesa zetu
.
Tunawaomba watanzania wote, kokote walipo duniani kuendeleza harakati za kutaka watuhumiwa wa wizi wa pesa za umma za akaunti ya Escrow wazirudishe. Pia katika ziara zitakazofanywa na chama nchi nzima wananchi wajitokeze kwa wingi kuunga mkono harakati na kudai pesa zao.

Deo Meck
 Mwenyekiti vijana Taifa 
Previous
Next Post »