Ofisa mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amefariki dunia na mwingine amesagika mguu baada ya mawe kuporomoka wakati wakipanda Mlima Kilimanjaro katika mazoezi.
Wanajeshi hao ni miongoni mwa maofisa 263 wa JWTZ waliopanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kwa makundi kuanzia Julai 12, mwaka huu kupitia njia ya Rongai iliyopo wilayani Hai.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 10:00 alfajiri katika urefu wa mita 5,000 kutoka usawa wa bahari wakati maofisa hao wakitoka eneo la Hans Meyer wakikaribia kilele cha Gilmans.
Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungulo alithibitisha jana kutokea kwa maafa hayo na kueleza kuwa mawe hayo yaliporomoka kutoka juu ya Hans Meyer na kushuka hadi eneo la Jamaica.
Aliyefariki dunia katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni Cadet MT 104948 Malata Thomas Kitene (26) baada ya kupata majeraha ya kichwa na Cadet MT 105896 Gabriel Makenge (32) ambaye amevunjika na kusagika mguu wa kushoto.
“Baada ya kupata taarifa za tukio hilo, kikosi chetu cha uokoaji kilikwenda eneo la tukio na kushiriki kazi ya uokoaji, lakini taarifa zaidi kuhusu ziara ya maofisa hao mnaweza kupata kwa wasemaji wa JWTZ,” alisema.
Hata hivyo, msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
Majeruhi pamoja na maiti ya ofisa hao waliteremshwa kutoka kileleni jana saa 4:00 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi.
Taarifa zaidi zilisema maofisa hao walipanda mlima huo ikiwa ni utaratibu wa kila mwaka kwa ajili ya mazoezi ya ukakamavu.
EmoticonEmoticon