WALIOMFUNGIA MTOTO NASRA KWENYE BOKSI MKOANI MOROGORO, WASOMEWA MASHITAKA YA MAUAJI

Mama mzazi wa Omari Mtonga, Devotha Dibagula wa pili kutoka kushoto akimwangalia mwanaye Omari Mtonga anayeangua kilio baada ya mahakama ya hakimu mkazi kuwabadilishia mashtaka kutoka yale ya kula njama na kumtesa Nasra Rashidi (4) wakati wa uhai wake na kuwa kesi ya mauaji yanayowakabili mama mkubwa wa Nasra Mariam Said wa kwanza kushoto na baba mzazi wa Nasra Rashid Mvungi kulia mara baada ya kuaghailishwa kwa kesi yao.


Ulinzi ukiwa umeimarishwa wakati watuhumiwa wakifikishwa mahakamani jana.
Mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mtoto Nasra Rashid Mvungi, Mariam Said ambaye ni mama mkubwa wa Nasra akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa jeshi la polisi mara baada ya kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Morogoro ambapo watuhumiwa watatu walibadilishiwa mashtaka kutoka kula njama na kumtesa Nasra Rashidi wakati wa uhai wake na kubadilishwa kuwa ya mauaji mkoani Morogoro.PICHA/MTANDA BLOG
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imewabadilishia mashtaka washitakiwa watatu katika kesi ya marehemu, Nasra Mvungi (4) waliokuwa wanakabiliwa na makosa ya kula njama na kufanya ukatili.

Sasa wanashitakiwa kwa kosa la kusababisha kifo cha mtoto huyo.

Watuhumiwa waliofikishwa katika mahakama hiyo ni pamoja na baba mzazi wa Nasra, Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe na mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro pamoja na wanandoa Mariam Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), wakazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, Mwendesha Mashitaka na Wakili wa Serikali, Sunday Hyera, kwa kushirikiana na wenzake, Wakili wa Serikali, Edgar Bantulaki na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Zabron Msusi, waliiomba Mahakama hiyo kuwasomea shitaka jipya la mauaji chini ya kifungu namba 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kwamba shitaka hilo halitawaruhusu washitakiwa kujibu lolote. 

Alidai mahakamani hapo kuwa katika tarehe tofauti ya mwezi wa Desemba mwaka 2010 hadi mei 2014 katika maeneo ya Kiwanja cha Ndege washitakiwa hao kwa nia ovu walimtesa mtoto Nasra Mvungi na kumsababishia kifo chake Juni Mosi mwaka huu. 

Hata hivyo, Hakimu Moyo alisema kwa mujibu wa sheria, Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shitaka hilo na hivyo kuiahirisha hadi Juni 26, mwaka huu itakapofikishwa mahakamani hapo kwa kutajwa tena. 

Watuhumiwa wote watatu walirudishwa rumande kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana.
Previous
Next Post »