Mtoto Fatuma Hassan (9) anyedaiwa kufungiwa ndani kwa siku tatu kisha kuchomwa moto mikononi na mama yake mkubwa aliyetajwa kwa jina moja la Diana (38), mkazi wa maeneo ya Tandale.
UNYAMA ulioje? Mtoto Fatuma Hassan (9) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Hekima iliyopo Tandale, Dar anadaiwa kufungiwa ndani kwa siku tatu kisha kuchomwa moto na mama yake mkubwa aliyetajwa kwa jina moja la Diana (38), mkazi wa maeneo hayo, kisa kikielezwa kuwa ni shilingi mia tano.
Tukio hilo lilitokea Juni 10, mwaka huu katika maeneo hayo ya Tandale Sokoni ambapo mama huyo alikuwa akiishi na mtoto wa mdogo wake kwa kile kilichodaiwa kuwa alimchukua kwa ahadi ya kumsomesha lakini kuna madai kuwa badala ya kufanya hivyo, alimnyanyasa.
Mama mkubwa wa mtoto Fatuma Hassan anyetuhumiwa kumtesa mtoto huyo.
Taarifa zilidai kwamba mama huyo aliamua kumfanyia ukatili mtoto huyo akidai kuwa alichukua fedha hizo akiwa na mwanaye wa kumzaa kwa ajili ya kwenda kutumia kununulia sambusa na juisi shuleni.
Ilisemekana kwamba kitendo hicho kilimkera mama huyo na kuamua kuwasubiri warudi ili awaulize kama kweli walichukua fedha hizo ambapo walikiri kuzitumia shuleni.
Wakizungumza na wanahabari wetu, majirani wa eneo hilo walisema kuwa walimuona mtoto Fatuma akipigwa na mama’ke huyo mkubwa fimbo na kumchoma moto mikononi pasipo kumpeleka hospitali huku akimpa onyo kali na kumfungia ndani.
Walisema kuwa mwanamke huyo amekuwa akimfungia ndani na kwenda kwenye genge lake.
Mjumbe wa eneo hilo, Said Sundi na Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Pakacha, Ally Mdee wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Wananchi walifikia hatua ya kufananisha tukio hilo na lile la mtoto aliyefungiwa kwenye boksi mkoani Morogoro, Nasra Mvungi (marehemu), walimkamata na kupiga simu katika Kituo cha Polisi cha Magomeni ambapo askari walifika na kumchukua mwanamke huyo.
Pia walimpeleka mtoto Fatma kwenye Hospitali ya Magomeni anakopatiwa matibabu huku mwanamke huyo akishikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na alifunguliwa kesi ya kujeruhi yenye jalada namba MAG/RB/5676/2014.
EmoticonEmoticon