ALIYEMLAZIMISHA MWANAFUNZI WA DARASA LA KWANZA KULA KINYESI CHAKE ATIWA MBARONI


JESHI la Polisi mkoani Geita, linamshikilia mkazi wa jijini humo Marco Maico (43) kwa kosa la kumlazimisha Mwanafunzi wa darasa la Kwanza, mwenye umri wa miaka (8) katika shule ya Msingi Nyakabale Wilayani Geita, kula kinyesi chake baada ya kukutwa akijisaidia karibu na kisima cha maji akiwa na wenzake wakati wakitoka shuleni. 

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Joseph Konyo, amehabarisha kuwaJuni 13, 2014 kuwa tukio hilo limetokea Juni 11, mwezi huu saa 4:45 asubuhi ambapo mwanafunzi huyo akiwa na wenzake watatu wakitoka shule kufanya usafi ,walipofika eneo hilo mwanafunzi mwenzao alienda kujisaidia karibu na kisima hicho kinachomilikiwa na Marco Maico.
 
Amesema mara baada ya mwanafunzi huyo alipomaliza kujisaidia ‘Marco’ alipita na kukuta kinyesi hicho na kuanza kumuamuru kuwa azoe kinyesi chake kwa mkono na kukitupa na baada ya kukitupa alimuamuru mwanafunzi huyo kukichukua na kukila hadi kiishe. Aidha, kutokana na hofu ya mwanafunzi huyo kuogopa kupigwa, alilazimika kukila huku wenzake wakimsubiri na baada ya kumaliza alienda nyumbani na wenzake.
 
Baada ya kufika nyumbani mwanafunzi huyo alimwambia Mama yake, Agnes Lujaja (26), juu ya tukio hilo ndipo Mama yake alipoenda kuripoti tukio hilo kwa balozi wa nyumba kumi kutoa taarifa na kupewa barua ya kumpeleka katika Zahanati ya Nyakabale kwa matibabu.
 
“Mara baada ya huyo Mama yake na mtoto kuripoti kwa Balozi wa nyumba kumi, ilikuwa bahati nzuri kwa kwa maana waliwahi kuripoti katika Kituo cha Polisi kilichokuwa karibu nao na ndipo tulipofuatilia tukio hilo kwa ukaribu na kufanikiwa kumkamata” alisema Konyo.
 
Hata hivyo, amesema baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia tukio hilo waliweza kumkamata mtuhumiwa ambaye hadi sasa anashikiliwa kwa upelelezi zaidi na kusema mara baada ya upelelezi kukamilika sheria itachukua nafasi yake.
Previous
Next Post »