Kimwaga apata mkosi mwingine

 Winga chipukizi wa Azam FC na Taifa Stars, Joseph Kimwaga ameumia tena goti baada ya juzi kuteleza na kuanguka wakati akitoka bafuni kuoga.
Kwa muda mrefu kinda huyo amekuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa na tatizo la goti kujaa maji na kumsababishia maumivu.
Akizungumza  Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa alisema tukio la Kamwaga kuumia limemshtua kocha wa timu hiyo Joseph Omog ambaye alikuwa na matumaini ya kuanza kumtumia katika mechi zijazo.
“Kimsingi hali ya afya ya Joseph Kimwaga ilikuwa inaendelea vizuri na jana (juzi) ilikuwa aanze mazoezi, lakini kwa bahati mbaya wakati anatoka kuoga aliteleza na kuangukia goti lile lile lililokuwa na matatizo.
“Kwa kweli kila mmoja hapa Azam amesikitishwa na tukio hilo hivyo kwa sasa tunajaribu kumtazama kwa siku mbili tuone kama hali itakuwa vilevile au pengine ni mshtuko tu,”alisema Mwankemwa
Alisema,”Kama hali yake haitatengemaa itabidi arejee kliniki kwa ajili ya matibabu zaidi.”
Wakati huo huo, Mwankemwa alisema tayari amepokea ripoti kutoka Afrika Kusini kuhusiana na uchunguzi wa tatizo la goti la beki wa timu hiyo Samir Nuhu na kuiwasilisha kwa bodi ya klabu yake.
Previous
Next Post »