Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu ya Young Africans leo imeichabanga bila huruma timu ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini Ruvu Shooting kwa mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo mwishoni mwa wiki iliiondosha kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika timu ya Komorozine de Domoni kutoka Visiwa vya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2 imeonyesha kwamba haikubahatisha kwenye ushindi huo ambapo leo imeendeleza makali yake.
Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la kwanza sekunde ya 40 ya mchezo kufuatia kupewa pasi nzuri na mshambuliaji Emmanuel Okwi ambaye aliwatoka walinzi wa Ruvu Shooting na kumpasia mfungaji ambaye hakufanya makosa.
Dakika ya pili ya mchezo Saimon Msuva aliipatia Young Africans bao la pili kufuatia kupewa pasi safi na kiungo Mrisho Ngasa ambaye leo alicheza kama kiungo mchezeshaji na kuwazidi ujanja viungo wa Ruvu na kumpatia mpira huo Msuva ambaye aliukwamisha mpira wavuni.
Akicheza mechi yake ya kwanza baada ya kuwa amedhuiliwa kwa muda na TFF, mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi aliipatia timu yake bao la tatu la mchezo dakika ya 27 kufuatia migongeo mizuri katii ya Msuva na Ngasa na mpira kumkua mfungaji ambaye hakufanya makosa.
Mrisho Ngasa ambaye leo alicheza kiungo aliwainua vitini washabiki wa Young Africans dakika ya 30 ya mchezo kwa kufunga bao la nne baada ya kuuwahi mpira mrefu aliopigiwa na mlinzi Mbuyu Twite na kumkuta Ngasa aliyewakimbiza walinzi wa Ruvu Shooting kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.
Ruvu Shooting walijaribu kufanya mashambulizi langoni mwa timu ya Yoiung Africans kupitia kwa washambuliaji wake Elias Maguri, Cosmas Lewsi na Jerome Lembele lakini mashamabulizi yao yakijikuta yakiishia mikononi mwa mlinda mlango Deogratias Munish "Dida".
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Ruvu Shoooting 0 - 4 Young Africans .
Kipindi cha pili kocha mkuu wa Young Africans Hans Van der Pluijm alifanya mabadiliko ambapo aliwaingiza Hassan Dilunga, Juma Abdul na Said Bahanuzi kuchukua nafasi za Mbuyu Twite aliyeumia, Mrisho Ngasa na Didier Kavumbagu.
Dakika ya 54 ya mchezo Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la tano la mchezo baada ya kumalizia krosi safi ya winga wa kulia Saimon Msuva aliyekua mwiba mkali kwa walinzi wa Ruvu Shooting.
Baada ya kukosa mabao ya wazi takribani matatu mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda Hamis Kiiza aliipatia timu yake bao la sita la mchezo dakika ya 70 kufuatia kumalizia kazi nzuri iliyofanya na kiungo Hassan Dilunga na Saimon Msuva.
Dakika ya 80 ya mchezo Saimon Msuva aliwainua tena vitini washabiki, wapenzi, na wanachama wa timu ya Young Africans baada ya kuipatia timu yake bao la saba la mchezo kwa shuti kali nje ya 18 kufuatia kuitumia vizuri pasi ya mshambuliaji Said Bahanuzi.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Ruvu Shooting 0 - 7 Young Africans.
Mara baada ya matokeo ya leo kocha mkuu wa Young Africans Hans Van der Pluijm amewapongeza vijana wake kwa kucheza vizuri, wamejituma kwa muda wote wa mchezo na kufuata maelekezo yake na kwa sasa anaamini moto ndo umeshaanza kuwaka kwa kila watakaokutana nao.
Young African simefikisha pointi 38 na kukamata tena usukuni wa Ligi Kuu huku ikiwa na mchezo mbele dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili Azam FC wenye pointi 36 na wakitazamiwa kucheza kesho dhidi ya timu ya Prisons.
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite/Juma Abdul, 3.Oscar, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Domayo, 7.Msuva, 8.Ngasa/Dilunga, 9.Didier/Bahanuzi, 10.Okwi, 11.Kiiza
SOURCE:YOUNG AFRICA
EmoticonEmoticon