JE UNAJUA LISHE INAYOMFAA MTOTO WA MIEZI 6-12 ?SOMA HAPA


Kwa miezi sita ya kwanza katika maisha ya mtoto chakula pekee ambacho wataalamu wa afya wanashauri apewe ni maziwa ya mama tu. Kunyonyesha ndio njia ya kwanza kabisa kumpa mtoto chakula. Unapoanza kumpa mtoto vitu vingine kama maziwa ya kopo wakati ana miezi michache utoaji wako wa maziwa unaathirika maana jinsi mtoto anavyonyonya ndivyo jinsi maziwa yanavyotengenezwa ndio maana watu wengi wanavyoanza kazi na kumuacha mtoto nyumbani maziwa yao yanaanza kupungua. Faida za kunyonyesha maziwa ya mama ni pamoja na:


  1. Maziwa ya mama yana virutubisho vingi vya asili ambavyo ni muhimu sana katika ukuaji na kinga kwa mtoto. Humlinda na magonjwa mengi ya utoto pamoja na ‘allergies’ mbalimbali.
  2. Hukuwezesha kuwa na ukaribu na mtoto wako.
  3. Hukupunguzia uwezekano wa kupata kansa ya matiti.
  4. Ni bure na unaweza kumpatia maziwa wakati wowote bila usumbufu.

Wakati gani Uanze Vyakula Vingine
Mtoto wako akifikisha miezi 6 unaweza kuanza kumpatia vyakula vingine kidogo kidogo ( Kuna ambao kutokana na sababu Fulani daktari huwashauri kuanza mtoto akiwa na miezi 4 hivyo ni  vyema ukiwasiliana na daktari wako kwanza). Mtoto akianza kupewa vyakula nje ya maziwa mapema kabla ya miezi 4 ni hatari kwa afya yake maana mfumo wake wa kusaga chakula unakuwa bado haujawa tayari. Unapoanza kumpa vyakula vingine hauachi kumnyonyesha, unyonyeshaji unaendelea hadi miaka miwili na nusu.
Dalili kuwa mtoto wako yupo tayari kuanza vyakula vingine ni:
  1. Amefikisha miezi 6
  2. Anaweza kushikilia kichwa juu ( shingo imekaza)
  3. Anaweza kukaa kwa kuwekewa kitu ( mfano kiti chenye mkanda)
  4. Unapompa chakula na kijiko anafungua mdomo kutaka kupokea au anageuza uso kwa kukataa
  5. Akipokea chakula anakiweka mdomoni na kujaribu kumeza na sio kukisukuma nje na kuacha mdomo wazi.
Hakikisha mtoto wako yupo tayari kabla hujaanza kumpa chakula na usimlazimishe sana anapoanza maana anaweza kuchukia chakula, inawezekana hapendi chakula ulichompa jaribu kubadilisha uone anapenda nini. Kila mtoto ni tofauti na mwingine hivyo usimlinganishe mtoto wako na mwingine la muhimu ni kuhakikisha kuwa anauzito kulingana na umri wake na anaongezeka kwa kupanda chati.
Mnapokuwa mnakula mezani mtoto naye awe hapo ili kumpa hamu ya kula na sio kila wakati akila anakuwa peke yake. Mpe chakula akiwa na furaha na pia akiwa na njaa ili aweze kufurahia chakula chake. Kabla ya kubadilisha aina ya chakula mpe kwa siku 3-4 mfululizo ili aweze kukizoea na kama kitamletea madhara ujue hasa ni chakula gani. Usimchanganyie vyakula maana hutajua anapenda nini na kuchukia nini na pia kama kuna kitu kitamdhuru ukichanganya hautagundua kwa urahisi.
Miezi 6-9
Endelea kunyonyesha na anza kumpa vyakula vyenye madini ya chuma. Mtoto alishwe kwa ratiba inayoeleweka kila siku na katika ratiba hiyo hakikisha angalau mara moja kwa siku muda wake wa kula unakuwa sawa na muda wa familia yote ili muweze kula pamoja. Vyakula vyake viwe vimepondwapondwa kabisa ikiwezekana tumia blender na hakikisha anapata mlo kamili yani matunda, mbogamboga, mbegu, nafaka, nyama na samaki. Inashauriwa kutokuchanganya aina tofauti za nafaka kwenye unga mmoja unapomtengenezea uji, uwe na unga wa mahindi, ulezi,mchele n.k tofauti tofauti. Pika aina moja ya uji kwa wakati unaweza kufanya kwa wiki au vyovyote utakavyopenda.
 Unapompa mboga au matunda anza na tunda moja moja kwa wakati. Osha vizuri matunda yako na katakata vizuri na kuponda ponda kisha mpe kiasi kidogo kwa wakati na kikibaki usikiweke, mtengenezee kile atakachokula tu. Matunda kama papai, parachichi na embe ni mazuri kwa kuanzia. Chemsha maharage, njegere au mboga za majani na kumpa supu kidogo kidogo, usiweke chumvi nyingi kidogo sana inatosha. Usimpe juisi za madukani, hakikisha unamtengenezea juisi wewe mwenyewe na usichanganye matunda mbalimbali kwenye juisi moja, na usiweke sukari kabisa.
Miezi 9-12
Katika umri huu mtoto anakuwa tayari amezoea ladha tofauti tofauti za vyakula mbalimbali nje ya maziwa. Anauwezo wa kukaa na kushikilia kitu kwa mikono yake na kuweka mdomoni hivyo anza kumpa matunda laini mkononi aanze kujifunza kula mwenyewe. Hakikisha vipande sio vidogo sana anavyoweza kumeza ili kuepuka hatari ya kukabwa. Kwa sababu pia atakuwa ameanza kuota meno atakuwa anapenda sana kutafuna tafuna. Katika umri huu pia unaweza kuanza kumpa kiini cha yai, ute wa yai hadi afike umri wa mwaka mmoja. Endelea kumnyonyesha ila kwa sasa anakula kwanza kisha ndio ananyonya maana akinyonya sana anaweza akakataa chakula. Usimpe chakula kimoja mfululizo kwa muda mrefu maana atakinai na kuanza kukataa chakula, mpe vyakula tofauti tofauti ili aendelee kupenda chakula.
Jinsi ya Kutengeneza Chakula cha Mtoto
Ni rahisi sana kutengeneza chakula cha mtoto nyumbani kwako. Osha mikono yako vizuri kabla ya kuandaa chakula na hakikisha unatumia vyombo visafi.
Matunda na mboga mboga: osha mboga zako vizuri kwa maji safi ( ya uvugu vugu) na kisha katakata na kubandika jikoni kwa chumvi kidogo sana bila mafuta. Ikichemka isage kwenye blender au ponda ponda iwe laini kabisa kisha mpe mtoto. Matunda osha pia kwa maji ya uvugu vugu, toa ganda la nje na kata vipande vikubwa kama unataka ale kwa mikono yake mwenyewe au ponda ponda na upe kwa kijiko.
Nyama na Samaki: Chemsha vipande vya nyama na maji kidogo na iive kwa moto wa kiasi hadi ilainike kabisa kisha isage kwenye mashine (food processor) na umpe na ile supu. Samaki vile vile ila samaki hakuna haja ya kuisaga maana ikiiva inalainika sana na ni rahisi kwa mtoto kula bila taabu (Kuwa makini sana na mifupa!).
Mbegu: Hapa nazungumzia maharage, kunde, choroko, njegere n.k Pika hadi ziive kabisa na kulainika kisha pondaponda na kumpa mtoto. Pia viazi na ndizi vinafaa sana kwa watoto, unaweza ukachanganya na supu ya samaki / nyama au na maziwa.
Nafaka: Usichanganye nafaka tofauti tofauti kwa ajili ya uji wa mtoto, inashauriwa kuwa na unga tofauti kwa kila nafaka. Unapopika uji unaweza kuweka karaga zilizosagwa ili kuongeza mafuta na vitamin kwenye lishe ya mtoto.
Usalama katika Kula
  1. Hakikisha haumuachi mtoto mdogo na chakula au kinywaji bila uangalizi hata kama ni maziwa ya chupa asije akapaliwa. Usimpe mtoto chakula au maziwa akiwa amelala, analia au anacheka.
  2. Usimpe chakula ambacho kinaweza kumkaba au kumpalia kama karanga, maindi, zabibu n.k
  3. Kabla ya kumpa mtoto chakula hakikisha umekiangalia joto lake usije ukamuunguza mdomo.
  4. Usafi wa mtayarishaji, mlishaji na mlishwaji ni muhimu san asana.
Mfano wa Ratiba ya Mlo wa Mtoto
Ratiba hii ni ya mfano tu, vyakula vilivyotenganishwa na / inamaana nikimojawapo kati ya hivyo. Hakikisha vyakula havichukui nafasi ya maziwa maana ni ya muhimu kwa afya ya mtoto wako
Previous
Next Post »