BASI LA BURUDANI LAUA 11 LAJERUHI ZAIDI YA 52 KOROGWE TANGA



 Basi  lenye namba za usajili T 610 ATR aina ya Nissan la kampuni ya Burudani ambalo  limepata ajali  leo na kuua watu 11 na kujeruhi zaidi ya 52 leo mkoani Tanga 

WATU 11 wamekufa  na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa vibaya baada  ya basi la abiria walilokuwa wakisafiria la Kampuni ya Burudani kutoka wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kuelekea Jijini Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka  .

 Ajali hiyo imetokea leo Disemba 12 mwaka huu majira ya saa 1.30 asubuhi  katika Barabara Kuu ya Segera Chalinze  eneo la Kwaluguru Kata ya Kwedizinga  wilayani Handeni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Constantine Massawe alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha gari lenye namba za usajili T 610 ATR aina ya Nissan.

Kamanda Massawe alisema kuwa majeruhi wa ajali hiyo wamefikishwa katika Hospitali ya wilaya ya Korogwe ya Magunga kwa ajili ya kupata matibabu .
Alisema dereva wa ajali hiyo Luta Mpenda(35) ni miongoni mwa watu wanaosadikiwa kufa na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Korogwe ya Magunga.
“Majeruhi wamekimbizwa katika hospitali ya magunga na hali zao bado siyo nzuri sana lakini na miili ya marehemu pia imehifadhiwa magunga”,alisema Kamanda Massawe.

Hata hivyo alisema kuwa chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo ambapo alipofika kwenye kona ya eneo la Kwalaguru gari lilimshinda na  kupinduka.

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo akizungumza kwa shida katika Hospitali ya Magunga alikolazwa Francis Bendera alisema kuwa kulikuwa na gari aina ya Fusso iliyokuwa wagongane nayo uso kwa uso ndipo dereva wa basi alipojaribu kukwepa gari hilo na badala yake kona ikamshinda na kupinduka.

“Tukiwa tunakaribia kwenye kona ile kuna fusso iliover take kwa speed kubwa sana na ilikuwa ije kutugonga uso kwa uso sasa dereva wa basi letu akawa anajitahidi kukwepa sasa kutokana na ile kona kuwa kali ndipo gari ilimshinda na kupinduka”alisema Bendera.

Nao baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa walisikia kishindo kikubwa katika eneo hilo na ndipo walipokaribia kufika kwenye eneo la tukio walikuta tayari gari imeshapinduka na baadhi ya watu kufa papo hapo.

“Sisi tulikuwa tumekaa huku ghafla tulisikia kishindo kikubwa kuja kukimbia kuangalia ndiyo tukakuta Basi la Burudani limepinduka lakini ile gari ilikuwa igongane uso kwa uso na fusso kusema kweli ile ajali ni mbaya sana”,alisema Zablon Mbaga.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa wilaya ya Korogwe ambao walifurika katika hospitali ya Magunga kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao na baadhi ya majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo walisema kuwa idadi kubwa ya abiria waliokuwa wakisafari katika basi hilo ni wafanyabiashara.

“Wengi hapa ni wafanyabiashara ndio wanaotumia basi hili kwa sababu wanauhakika wakiondoka alfajiri saa 12 wanaweza kufika Dar mapema na kugeuza jioni”,alisema Fatuma Bakari mkazi wa wailaya ya Korogwe
Mpaka sasa idadi ya majeruhi waliotokana na ajali hiyo imefikia 55 ambapo imemlazimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo kuanza zoezi la uhamasihaji wa utoaji damu kwa wananchi ili kuwanusuru wagonjwa hao ambao hali zao ni mbaya.

Akizungumza katika mahojiano na mtandao huu wa matukiodaima.com Gambo alisema kuwa majeruhi wengi wamepoteza damu nyingi hivyo mahitaji ya damu yamekuwa makubwa ukilinganisha na akiba iliyopo hospitalini hapo.

“Majeruhi wengi wamepoteza damu nyingi sana na sasa kilichopo tunahamasisha wananchi wajitolee damu ili tuweze kunusuru hali kwani ni mbaya sana”,alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya akiwa ni miongoni mwa watu wanaoshughulikia kuwapa huduma ya kwanza wagonjwa hao.

Hata hivyo alisema kuwa tayari majeruhi wanne wa ajali hiyo wameshasafirishwa kupelekwa katika Taasisi ya mifupi ya Moi kwa ajili ya matibabu zaidi.
MWISHO
SOURCE:Francis Godwin Mzee wa Matukio
Previous
Next Post »