Hatimaye wasanii nyota wa muziki wa dansi Tanzania Ally Choki ‘Freemason’, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone a.k.a Mwalimu wa walimu’ na Mwinjuma Muumin ‘Kocha wa dunia’ wameamua kurudisha umoja wao uliowahi kuvuma wa Mafahari watatu.
Nguli hao tayari wameanza mazoezi makali ya muziki pamoja huku kila mmoja akijinasibu kuwa umoja huo utatikisa nchi.
Mtandao huu uliweza kuwanasa mastaa hao ndani ya uumbi wa Meeda Sinza jijini Dar es Salaam wakiwa katika mazoezi makali ya pamoja sambamba na wasanii wa bendi ya Extra Bongo, huku tajiri Chief Kiumbe ‘Big Boss’ ikidaiwa ndiye aliyewaunganisha tena.
Choki aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli wameamua kuunganisha nguvu ambapo watakuwa wakifanya maonesho mengi pamoja wakianzia na maonesho ya msimu huu wa Sikuukuu.
“Nadhani mashabiki wetu wanaelewa tunapozungumzia maana ya Mafahari watatu.Ni Banza Stone, Muumini na mimi Ally Choki.Kwa kuanzia maonesho yetu tutafanya mpambano mkubwa sana siku ya mkesha wa Krismasi ndani ya ukumbi wa Meeda Club Sinza jijini Dar es Salaam ambapo siku hiyo tutamtafuta mkali wa dansi baina yetu” alisema Choki.
Aliongeza“ Krismasi itakuwa fainali ambayo itafanyika ndani ya ukumbi wa kisasa wa Miti Mirefu Sayansi Kijitonyama . Siku hiyo Muumini, Banza na mimi tutashambulia jukwaa mfurulizo na atakaye pagawisha mashabiki ndiyte atakayeibuka fahari dansi” Alisema kuwa onesho hilo kwa wapenzi wa muziki wa dansi siyo la kukosa kabisa kwani litakuwa ni onesho la kufunga mwaka.
Naye Muumnini Mwinjuma alibainisha kuwa anajisikia fahari sana kufanya kazi na wababe wenzake na kwamba mashabiki wasubiri kuona shoo za maana.
Baada ya kuzindua maonesho yao jijini Dar es Salaam Mafahari hao Watatu watauhamishia mpambano wao Geita wakati wa mkesha wa mwaka mpya ambapo mpambano huo utalindima ndani ya ukumbi wa Omega Sprendid huko na siku ya Mwaka mpya yenyewe na Januari 2 mpambano utahamia Kahama. “Tumeamua kupeleka huko kutokana na maombi ya mashabiki wetu .Hivyo basi watu wa Kahama na Geita wajiandae kupata shoo kali kutoka kwa Banza Stone, Muumini na Ally Choki wakishambulia jukwaa pamoja” alisema Choki.
EmoticonEmoticon