ASEMA
MADAI YAO YANAZUNGUMZIKA WASIANDAMANE
HATIMAYE Rais Jakaya
Kikwete amekata mzizi wa fitina kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya
katiba unaopigiwa kelele na vyama vya siasa na wadau, akiwataka warudi mezani
kujadiliana na serikali.
Rais Kikwete alitoa
rai hiyo jana katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita akisema: “Kama
dhamira yetu ni kutaka kupata katiba mpya kwa mujibu wa katiba na sheria,
ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa
waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia.”
Badala yake aliwataka
watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za
kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha sheria ya marekebisho ya
sheria ya mabadiliko ya katiba.
“Tukifanya hivyo tutakuwa
tunajenga badala ya kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika serikali tuko
tayari,” alisema.
Katika hotuba hiyo,
pia aligusia masuala mbalimbali kama vile operesheni ya kuwaondoa wahamiaji
haramu nchini, shambulio la kigaidi nchini Kenya na mafanikio ya ziara yake nje
ya nchi.
Alisema kuwa hivi sasa
tume inaandaa mapendekezo ya rasimu ya pili ya katiba itakayopelekwa kwenye
Bunge Maalumu.
Kwamba baada ya
tafakuri zake, Bunge Maalumu litatoa rasimu ya mwisho ya katiba ambayo
itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Alisema kuwa baada ya
Bunge la Novemba, 2011 kupitisha sheria ya mabadiliko ya katiba, kulikuwepo na
madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo
vyama vya upinzani na chama tawala.
“Majadiliano
yalifanyika baina ya serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za
kiraia. Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu,” alisema.
Kwa mujibu wa rais,
awamu ya kwanza ilihusisha Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike
marekebisho yanayohusu Bunge Maalumu na mwisho kura ya maoni.
Alisema kuwa kama
ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii
nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.
Kwamba yalifanyika
mazungumzo kati yao na serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya
kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya muswada na kuuwasilisha
kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba
uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.
“Pili walishauri
kwamba kama Bunge Maalumu litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa,
liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90,” alisema.
Alisema kwa kuzingatia
utaratibu wa kutunga sheria, serikali ilifikisha muswada kwa Spika wa Bunge
ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala.
Kama ilivyo ada,
kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu muswada. Kwamba
aliambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na
wadau.
Alisema kisha wajumbe
wa kamati walikaa wenyewe kujadili muswada, wakiwepo pia wabunge ambao si
wajumbe wa kamati walioshiriki kwa vile kanuni zinaruhusu.
“Nimeambiwa pia kwamba
mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na
wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya muswada,” alisema.
Rais aliongeza kuwa
alifahamishwa kuwa wabunge wa vyama vyote walichangia, na kwamba baadhi ya
nyakati mambo yalipokuwa magumu mawazo mazuri ya baadhi ya wabunge wa upinzani
yalisaidia kupata ufumbuzi.
Alisema kuwa aliambiwa
pia kwamba wajumbe wa kamati na upande wa serikali walikubaliana kwa maeneo
mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke bungeni ili
wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Kwamba baada ya kamati
kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe aliwasilisha
muswada bungeni, akifuatiwa na Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya kamati.
Baadaye Msemaji wa
Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alitoa maoni yake. Kuwa baada ya watu hao watatu
kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa wabunge wangeanza kujadili muswada.
“Naambiwa mambo
hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya
wabunge wa upinzani wakitaka muswada usijadiliwe.
“Ilifikia wakati hoja
hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali isiyotarajiwa,
wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili,” alisema.
Rais alisema kitendo
hicho kimewanyima wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao
walizozitoa kupitia hotuba ya msemaji wao, na kwamba walijinyima nafasi ya
kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Alisema uwa wabunge
waliokuwepo waliendelea kuujadili muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya
kuuboresha.
“Walifanya hivyo
wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi ya hoja na
mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa
ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na lile la ukomo
wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa maoni yangu madai
ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama
wabunge wake wangekuwepo bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na
kupitisha miswada bungeni.
“Baada ya kupoteza
fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.
Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa bungeni na si
vinginevyo,” alisema.
Alisema kuandamana
nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA,
Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria
hiyo.
“Naomba hekima
ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia
utaratibu tulioutumia mwaka 2012.
“Kulipotokea mazingira
kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na
kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua
zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo,” alisema.
Aliongeza kuwa kufanya
kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na kutaliingiza taifa kwenye
matatizo yasiyokuwa ya lazima.
“Tukikataa kufanya
hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia
zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata katiba mpya
kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine
iliyojifisha?” alisema.
Rais Kikwete
alisisitiza kuwa hawatengenezi katiba ya chama fulani bali katiba ya nchi,
katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko
wote.
“Lazima tuongozwe na
ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si
watu wote wanaostahili au kuwa na sifa, ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa
wajumbe, hivyo wale wachache watakaobahatika lazima wawasemee wote,”
alisema.
Ushirikishwaji
wa Z’bar
Katika hilo, rais
alisema kuwa alieleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ilivyoshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika muswada.
“Hivyo basi napata
tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa
msingi wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa,” alisema.
Alisema kuwa aliulizia
kuhusu hoja ya kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau,
akaambiwa kuwa kanuni za Bunge hazina sharti hilo, hivyo kamati haistahili
kulaumiwa.
“Kama hivyo, nashauri
kuwa suala hili lirudishwe bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia
uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulaumiana isivyostahili,” alisema.
Alisema kuwa aliambiwa
pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Rais alifafanua kuwa
ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi
imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia.
Alisema kuwa Bunge
Maalumu lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande
kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
“Hivyo basi, katika
Bunge Maalumu nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata, bali
ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda
maslahi ya Zanzibar,” alisema.
Alisema kuwa anadhani
inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama wabunge wataamua waongeze idadi, itakuwa kwa
sababu nyingine siyo hiyo ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume
ya Warioba
“Katika orodha ya
madai ya ndugu zetu wa upinzani, lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka
usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalumu bali waendelee kuwepo
mpaka mwisho wa mchakato.
“Nimeulizia ilikuwaje?
Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya serikali wala ya Kamati
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la mbunge katika
Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
“Kwa hiyo kuilaumu serikali
si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii. Nami naiona hoja ya
wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalumu hasa wa kusaidia
kufafanua mapendekezo ya tume,” alisema.
Alihoji kuwa ushiriki
huo uwe vipi? Je, ni wajumbe wote au baadhi yao na kusema kuwa hilo ni jambo
linaloweza kujadiliwa.
EmoticonEmoticon