Mkakati wa kusajili watoto chini miaka mitano waanza



Wakala  wa Usajili na Ufilisi (Rita), imeanzisha mkakati wa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano ili kuondoa usumbufu na msongamano ambao umekuwa ukijitokeza. Pia kuhakikisha idadi kubwa ya Watanzania wanaostahili kuwa na vyeti hivyo wanavipata kwa wakati badala ya kusubiri. 

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Rita, Joseph Kimaro, alisema jijini Dar es Salaam  kuwa mkakati huo ulianza tangu Julai, mwaka huu mkoani Mbeya na unatarajiwa kupelekwa katika mikoa mingine. Alisema pia mkakati huo umelenga kuondoa ada ya cheti katika kundi hilo ili kuhakikisha asilimia kubwa ya watoto wanapatiwa vyeti.

Mbali na kundi hilo, pia alisema wanatarajia kuanza mkakati mwingine hivi karibuni wa kusajili na kutoa vyeti katika shule za msingi kwa kuanza na Mkoa wa Dar es Salaam.

Kadhalika, alisema mkakati huo umeanza kufanyika kwa makundi maalum na kwamba tayari wamekuwa wakipatiwa vyeti katika maeneo waliko pale wanapohakikiwa kuwa wana sifa za kupatiwa vyeti hivyo.

Kimaro aliongeza kuwa miaka ya nyuma, wananchi walikuwa wanatumia muda mwingi sana kufuatilia vyeti vya kuzaliwa kutokana na mfumo uliokuwapo, lakini hivi sasa wametatua tatizo hilo baada ya kuboresha baadhi ya mifumo.
Previous
Next Post »