Mlemavu afichwa ndani kwa miaka 12






Leba  akiwa na mama yake.
Ni umbali wa kilomita saba kutoka katikati ya Mji wa Dodoma upande wa Mashariki barabara iendayo Morogoro, kipo kijiji maarufu cha Nzuguni.
Miaka ya hivi karibuni kijiji hiki kimevuma katika vyombo mbalimbali vya habari kutokana na mambo makubwa matatu.

Mosi ni eneo la Maonyesho ya Siku kuu ya wakulima Nane Nane na pili eneo lililovuma kwa machimbo ya dhahabu lakini pia ndipo yanapojengwa majengo ya Chuo Kikuu cha Polisi.

Pamoja na ukaribu wake na umaarufu huo ukiachia mbali kuzungukwa na eneo la Mradi wa Ujenzi wa Uwanja Mkubwa wa ndege, na mradi wa Chuo cha Biashara, ndani ya kijiji hicho kuna vituko na wakati mwingine ni mikasa isiyoelezeka.

Wapo wanaofurahia maisha, lakini wapo ambao hawajui na hawana matumaini wakati wote, wapo mradi wapo.

Katika Mtaa wa maarufu wa Mapinduzi iko familia ambayo wakati mwingine kwa mtu wa kawaida unaweza usiamini simulizi yake lakini ni ukweli mtupu kwamba kuna tatizo katika familia hiyo jambo ambalo linahitaji juhudi za makusudi kuwasaidia.

Waswahili wanasema ‘kama hujui kifo basi kachungulie kaburi’ hivyo basi, hali ya maisha ya familia hii kwa ujumla inahitaji kusaidiwa, wanaishi kwenye katika kibanda kidogo cha tope.
 

Ni katika familia ya Lameck Mwitewe Senyagwa na mkewe Anastazia Alfred yupo Stephen Lameck (21), kijana ambaye hajui mwanga wa jua la kijiji hicho ukoje, wala haijulikani ni lini kijana huyo ataishi walau kama binadamu wengine.

Stephen (Leba) ni mtoto wa kwanza katika familia ya  watoto wanne wote wakiwa wa kiume, lakini yeye pekee ndiye ambaye hajawahi kuyafaidi maisha katika kipindi chote cha uhai wake.

Ni mlemavu wa miguu, mgongo na hazungumzi chochote ingawa kwa ishara anaweza kueleza nini anachotaka kutendewa wakati huo.

Kwa namna ilivyo, angeweza hata kuendesha baiskeli ya miguu mitatu, lakini nani wa kumpa baiskeli hiyo ili imsaidie kijana huyo kuona mwanga wa jua, ni tabu na mateso makubwa juu yake.

Nilifika katika kibanda kidogo ambacho familia hiyo ya watu sita (watoto wanne na wazazi wawili wanaishi), inatia huruma lakini ndiyo hali halisi waliyo nayo, na haikuwa mara ya kwanza kuona maisha duni kama hayo isipokuwa mateso yapo kwa Stephen.

Previous
Next Post »