Tumeshtushwa
mno na kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wiliam Lukuvi
kwamba wabunge wengi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wanatuhumiwa
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuonya kwamba iwapo
Serikali italazimika kuwataja hakuna mbunge yeyote atakayesalimika.
Waziri
Lukuvi ambaye anashughulikia masuala ya Bunge alitoa kauli hiyo bungeni
juzi wakati akijibu maswali ya nyongeza ambapo wabunge waliitaka
Serikali kutaja majina ya vigogo wanaojihusisha na biashara hiyo.
Mmoja wa
wabunge hao alimuuliza kama Serikali inaweza kuwaeleza Watanzania kuhusu
ukubwa wa biashara hiyo nchini, wakati mbunge mwingine alihoji sababu
za Serikali kushikwa kigugumizi kila inapotakiwa kutaja majina ya
magwiji wauza 'unga'.
Zipo
tetesi kuwa, kauli ya waziri huyo kwamba wabunge wengi wanatuhumiwa
kujihusisha na biashara hiyo inaweza kuwa imetolewa kama mbinu ya
kuwanyamazisha wabunge ili waingiwe hofu na kujenga dhana kwamba hakuna
mbunge miongoni mwao aliye msafi.
Hatudhani
kama ungekuwapo utata iwapo waziri huyo angesema baadhi ya wabunge
wanadaiwa kufanya biashara hiyo, kwani wananchi wengi wamekuwa wakijua
jambo hilo kwa muda mrefu. Siyo siri kuwa, kwa muda mrefu baadhi ya
wabunge walikuwa wakitajwa kujihusisha na biashara hiyo hata kabla
hawajaingia bungeni.
Hata
hivyo, yafaa ieleweke kwamba jambo linalogomba hapa ni kauli kwamba
wabunge wengi wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo. Ndio maana
tunadhani kuwa, hakuna anayeweza kubisha kwamba kauli ya Waziri Lukuvi
ni nzito mno na inaliweka Bunge njia panda kwa wabunge wake wengi
kukabiliwa na tuhuma nzito kama hizo.
Ni kauli
ambayo bila shaka imechafua taswira ya Bunge machoni mwa wananchi na
imeibua maswali mengi kuhusu hadhi ya Bunge na wabunge wenyewe.
Pengine
ndio maana baadhi ya wabunge walimtaka Waziri Lukuvi kufuta kauli yake
hiyo kwa maelezo kwamba siyo tu ni ya jumla mno, bali pia kwamba
imelichafua Bunge. Bila shaka wabunge hao walitaka kuonyesha kwamba wao
ni wasafi, hivyo tunadhani hawakutendewa haki kwa kulundikwa katika kapu
moja na wabunge waovu.
Tunadhani
kauli ya Waziri Lukuvi kwamba iwapo Serikali italazimika kuwataja
watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya hakuna mbunge atakayesalimika
haikuwa ya busara na ilitolewa tu kwa kukurupuka baada ya wabunge
kumzomea.
Vinginevyo,
Waziri alipaswa kujua unyeti wa suala hilo hasa kwa kutilia maanani
kwamba Rais Jakaya Kikwete miaka minne hivi iliyopita alisema ana orodha
ya magwiji wa 'unga' , lakini hadi leo hajapata ujasiri wa kuyaweka
bayana.
Kwa
misingi hiyo, nani anaweza kuamini kwamba Waziri Lukuvi alitoa kauli
hiyo kwa nia njema? Tunasema hivyo kwa sababu kauli hiyo ilijenga dhana
potofu kwamba wabunge wote, wakiwamo Spika, Waziri Mkuu na mawaziri
wanajihusisha na biashara hiyo haramu.
Ni kauli
ambayo tunaweza kusema inadhihirisha kwamba Serikali sio tu imekata
tamaa katika vita dhidi ya biashara hiyo, bali pia kwamba sasa iko njia
panda na haijui nini la kufanya.
CHANZO MWANANCHI.
EmoticonEmoticon