Mama Tunu Pinda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma ya kumsadia mtoto wakike kushoto kwake ni mkururugenzi Mtendaji wa Tmarc Bibi Diana Kisaka ambao ndio wandaji wa mradi huo kulia kwa mama pinda ni Ludovicka Tarimo mshauri wa maswala ya jinsia kutoka USAID anayefuatia ni Mkuu wa voda com Foundation Bwana Yessaya Mwakifulefule sherehe hizo zimefanyika mkoani Mtwara: picha na Chris Mfinanga
MKE WA
WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania washirikiane na wazazi
na walimu kuhakikisha watoto wa kike wanasoma kwa bidii na kutimiza
ndoto zao za ukubwani.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 20, 2013) wakati akizindua Mradi
wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko
Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara. Mradi huo unafadhiliwa na
Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo,
umelenga kuwafikia wasichana 10,513 katika wilaya mbili za mkoa wa
Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Kabla ya
kuzindua mradi huo, Mama Pinda aliwaita wasichana watatu na kupanda nao
jukwaani na kuwahoji mmoja baada ya mwingine kwamba wangependa kufanya
nini wakiwa wakubwa.
Mwanafunzi
wa kwanza, Rahma Jamaldini (14) anayesoma darasa la saba katika shule
ya msingi Chikongola alijibu kwamba yeye angependa kuwa rubani na
akaambiwa na Mama Pinda ajitahidi katika masomo ya sayansi na hisabati
ili asome hadi Chuo Kikuu kuweza kutimiza ndoto yake hiyo.
Wa pili
alikuwa ni Eliza Paulo (8) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya
msingi Chikongola aliyesema angependa kuwa mama. Aliwavunja mbavu watu
waliohudhuria uzinduzi huo alipoulizwa tena ni kitu gani angependa
kufanya mbali ya kuwa mama kwa kujibu kwamba angependa kupika.
Alipoulizwa mara ya tatu kitu kingine ambacho angependa kufanya, akajibu
kuosha vyombo. Mama Pinda allimhimiza asome kwa bidii ili awe mama
mzuri.
Wa tatu
alikuwa ni Bora Hamisi (8) ambaye pia ni mlemavu wa ngozi. Bora anasoma
darasa la pili katika shule ya msingi Msufini mjini Mtwara. Yeye alisema
angependa fundi wa kushona nguo. Naye aliambiwa asome kwa bidii hasa
somo la stadi za kazi.
Mama
Pinda alisema amewaita watoto hao ili wawe mfano wa kudhihirisha ndoto
na matamanio ambayo watoto wa kike wanayo na kwamba wasiposaidiwa kwa
kuwekewa mazingira mazuri yatakayowafanya wahitimu masomo yao, kamwe
hawataweza kutimiza ndoto zao.
"Watawezaje
kutimiza ndoto zao kama hawahudhurii masomo kama wanafunzi wengine?
Wanapaswa wasome vizuri, waende sekondari na hata vyuo vya elimu ya juu.
Tuweke miundombinu itakayowasaidia kuhudhuria masomo bila kukosa,"
alisema.
Mapema,
Mkurugenzi Mtendaji wa TMARC, Bi. Diana Kisaka alisema mradi huo
umelenga kuinua uelewa wa wasichana kuhusu miili yao na mabadiliko
yanayotokea katika kipindi cha balehe; kuwapa ufahamu kuhusu makundi
mbalimbali miongoni mwa jamii iliyowazunguka na kuwapa upeo wao kuhusu
umuhimu wa kuzingatia malengo yao katika maisha.
Naye Mkuu
wa Vodacom Foundation, Bw. Yesaya Mwakifulefule alisema Vodacom
Foundation imechangia sh. milioni 160 kwenye Mradi wa Hakuna Wasichoweza
kwani inatambua umuhimu wa elimu na suala zima la kuendeleza wasichana
kielimu.
"Vodacom
Foundation inashugulika na masuala ya elimu kwa kuchangia madawati na
teknolojia ya habari na mawasiliano katika shule mbalimbali hapa nchini.
Hapa Mtwara tumetoa kompyuta 20 kwenye shule ya sekondari ya wasichana
ya Mtwara ambazo zimeunganishwa na intaneti ya Vodacom," alisema.
Naye
mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Maendeleo la Marekani (USAID),
Bi. Ludovicka Tarimo, alisema taasisi yake imechangia Dola za Marekani
196,650 kwenye mradi huo ambao wanaamini kupitia utekelezaji wake,
utawasaidia mamilioni ya watoto wa kike hapa nchini kupata mafunzo ya
kujitambua na hatimaye kufanikiwa kielimu
EmoticonEmoticon