MAJINA 8,805 YAKATALIWA TCU

blogger-image-1885083474 9b6ea

Hussein Makame, MAELEZO

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imekataa kuyachagua majina ya wanafunzi 8,805 walioomba kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza kwenye fomu zao za maombi.

hdg

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Sifuni Mchome, wanafunzi hao hawakuchaguliwa na tume hiyo kujiunga na vyuo vikuu kutokana na maombi yao ya programu zote walizochagua kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa.

Ilieleza taarifa hiyo kuwa sababu za kutochaguliwa kwa wanafunzi hao ni pamoja na ushindani wa wanafunzi katika programu walizochagua, wanafunzi kushindwa kuwasilisha programu walizochagua na kuchangua programu ambazo hawana sifa nazo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imewapa nafasi nyingine wanafunzi hao kuomba tena kwa awamu ya pili kwa kuchagua programu nyingine ambazo wana sifa nazo kupitia mfumo wa udahili wa TCU ambao umeshafunguliwa tangu Julai 29 hadi Agosti 9 mwaka huu utakapofungwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanafunzi anatakiwa kuangalia jina lake katika orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaliwa na TUC, orodha inayopatikana kwenye tovuti ya taasisi hiyo ya www.tcu.go.tz na kufuata utaratibu uliowekwa kuomba upya.

"Baada ya mwanafunzi kuthibitisha jina lake kwenye orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa iliyoko kwenye tovuti ya TCU, unatakiwa kufuata masharti yafuatayo, chagua program moja tu kutoka kwenye orodha ya programu inayopatikana kwenye tovuti ya TCU" alisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa masharti hayo, pia mwanafunzi anatakiwa kufungua muongozo wa udahili unaopatikana kwenye tovuti hiyo na kuthibitisha kwamba anayo sifa stahiki ya kujiunga na programu aliyoichagua.

Masharti hayo pia yanamtaka mwanafunzi ambaye hakuchaguliwa, kuingia kwenye sehemu ya taarifa za mwanafunzi (profile) kwa kuingiza jina analotumia na namba yake ya siri, kubofya kitufe cha kuomba, kuchagua programu moja tu, kubofya kwenye makasha ya kuthibitisha na hatimaye kuwasilisha maombi yake.

"Baada ya kuwasilisha maombi yako mfumo wenyewe utakutaarifu kuwa ama unastahiki kuomba programu hiyo au la, na uchaguzi utaegemea kwenye msingi wa wa kwanza ndiye atakayehudumiwa mwanzo"ilisisitiza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa:

"Pindi programu moja itakapojaa, haitaoneshwa kwenye orodha ya programu zinazohitaji kujazwa kwenye mfumo wa udahili, hivyo utahitajika kujaza programu nyingine"

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwisho wa kutuma tena maombi hayo ni Agosti 9 mwaka huu na iwapo mwanafunzi atapata tatizo kuhusu maombi hayo atatakiwa kuwasiliana na TCU kwa anuani au kupiga simu namba 0757 593868; 0757 594087; 0656 596822 na 0682 544832 au afike kwenye ofisi za tume zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam.

mwisho

Previous
Next Post »