Mtoto amkatakata mamaye kinyama

Na Lilian Mkusa, Njombe
WIKI iliyopita katika Mtaa wa Maheve uliopo Kata ya Ramadhani mkoani Njombe yalitokea mauaji ya kutisha yanayomhusisha mtoto aliyemkatakata mama yake mzazi kwa shoka kutokana na kugombania mirathi.
Baada ya kufuatilia kisa hicho cha kutisha, kwa kuwasiliana na ndugu wa marehemu, Serikali ya Mtaa na taarifa kwenye mazishi ya mama huyo, Ferejina Mligo (65), Daraja Letu limesimuliwa namna kijana alivyomtoa mama yake roho.
SeMlowe, ambaye ni binamu wa marehemu, anaeleza kuwa kijana huyo, Fiano Mgeni (26) alifanya kitendo hicho cha kinyama Jumatatu Mei 20, 2013, nyumbani kwao Mtaa wa Maheve.
“Fiano alimvamia mama yake na kuanza kudai kuwa kwa nini ameuza eneo la familia lililokuwa na milingoti mitatu bila taarifa?”anasema SeMlowe.
Inaelezwa kuwa, mama huyo alijaribu kujitetea kwa kueleza kuwa suala hilo tayari lilishajadiliwa kifamilia na kufikia muafaka, lakini kijana huyo aliendelea kumfokea na kumpiga na shoka katika maeneo yake ya mwili.
“Tulikuwa kijiweni ghafla Fiano akaja na akawa anajitapa kwamba ameua, amemaliza kazi kwa manufaa ya wengi,” anasema mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Grewn Mtulo, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Maheve, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mpaka sasa mtuhumiwa anashikiliwa na polisi huku taratibu nyingine zikiendeelea kufuatiliwa.
“Suala hili ni zito, tutaandaa mkutano wa hadhara tuzungumze na vijana juu ya tabia hizi za kikatili zinazoendelea kwa sababu zinaturudisha nyuma kimaendeleo,” anasema kiongozi huyo.
Previous
Next Post »