Mh. Mukangara awataka vijana wa Kitanzania kushiriki kambi ya dunia ya vijana itakayofanyika jijini Dar

Picha-na-1

Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara (pichani) amewashauri vijana nchini kushiriki  kambi ya Dunia ya vijana inayotarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi huu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Waziri Dkt. Mukangara ameutoa ushauri huo hivi karibuni wakati akiongea na vijana wa kikundi cha Mambo Safi kilichopo Kata ya Kimara jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa vijana kushiriki kwao katika kambi hiyo kutawawezesha kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na utamaduni wa watu kutoka nchini Korea na China, pia watakutana na watu kutoka mataifa mbalimbali ambapo wataweza kubadilishana mawazo na hivyo kujengeka kifikra.

Kwa upande wake Viola Massawe kutoka  International Youths Fellowship  (IYF) amesema kuwa malengo waliyonayo ni kuwakutanisha vijana 2000 katika maudhui ya badilisha FIKRA kutoka mtazamo hasi kwenda mtazamo chanya pamoja na tamasha la Muziki wa Cantata.

Massawe amesema kuwa mshiriki wa mkutano huo ambaye ni kijana anatakiwa kulipia kiingilio cha  shilingi 10,000/=   kwa gharama hizo atapataT-shirt, kitabu , chakula na malazi kwa muda wa siku tano na  cheti pindi atakapomaliza mafunzo.

Amesema “Kutakuwa na hotuba na mafundisho kuhusu elimu ya ufahamu, tamasha la muziki za Gracias kwaya, michezo ya utamaduni ya kimataifa, masomo ya Academy kwa lugha za Kispanish, Kichina, Kirussia, Kikorea, Kiingereza, TAE-KWON-DO na Marathon”.

Kambi hiyo inaandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na International Youths Fellowship  (IYF) itaanza tarehe 29 Julai, hadi tarehe 2 Agosti mwaka huu.

Kambi ya vijana imekuwa ikifanyika nchini kuanzia mwaka 2009 kwa mwaka jana vijana 1000 kutoka pande zote za Tanzania waliweza kushiriki huku wengi wao waliweza kuishi maisha mapya kupitia kambi ya IYF  kwa kupewa fikra ya maana na mtazamo chanya juu ya mambo ya maisha yao.

Previous
Next Post »