Askofu Charles Gadi wa Good News For All Ministry atoa sababu ya timu ya taifa kukosa ushindi dhidi ya Ivory Coast.

 

gadi

Maaskofu na Wachungaji wa Good News For All Ministry wametoa sababu ya Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kukosa ushindi katika mechi yao naTimu ya Ivory Coast iliyofanyika jumapili iliyopita Juni 16, mwaka huu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari – MAELEZO  jijini da res salaam, Askofu Charles Gadi amesema kuwa kuna sababu nyingi zilizopelekea Taifa Stars kushindwa katika mchezo wake na Ivory Coast ikiwa ni pamoja na matusi na mzaha unaofanywa na wananchi wenyewe.

 

“Ndugu waandishi, ni kweli goli la kwanza lilifungwa kwa maombi ya Watanzania waliokuwa wakiomba, lakini matusi yaliyoendelea pale uwanjani ambayo yanatukana maumbile ya mama, dada, wakwe na watoto zetu wa kike yalitukwamisha.

 

Askofu Gadi amesema “ Unapotukana kwa kutumia maumbile ya wakina mama ni sawa na kuchafua, kukejeli uumbaji wa Mungu kwa wakina mama, hali hiyo hutuletea laana ya kushindwa,”.

 

Ameongeza kuwa walianza kuiombea Taifa Stars toka mwaka 2012 ili ifanikiwe katika mechi zake zote, hivyo wana uchungu kwa kufungwa na timu hiyo ya kigeni.

 

Aidha Askofu Gadi ameongeza kuwa pale uwanjani kulikuwa kumefurika watu wengi hivyo kuhatarisha usalama wa watu walioko pale na hivyo ameliomba  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litoe tiketi kulingana na idadi ya viti vilivyopo uwanjani.

 

Pia Askofu Gadi amesema kuwa wana maombi ya siku elfu moja kwa ajili ya kuliombea Taifa zima, mpaka sasa wamekaribia siku mia tano katika maombi  hayo hivyo wanaomba watu kutokwamisha maombi yao kwa kuacha matusi.

 

Naye Mchungaji Leonard Kijuna amesisitiza kuwa “Naomba Watanzania wamwogope Mungu kwa kuacha matusi na dhambi zao kwani wakifanya hivyo nchi itakuwa na maendeleo na kuwa ya kistaarabu kwa kuendeleza amani,”.

 

Pia Askofu Gadi ametoa wito kwa Serikali kutunga sheria kuhusu matusi, kwamba endapo mtu atapatikana akitukana basi achukuliwe hatua kama zilivyo nchi njingine, mtu akitupa bigijii anafungwa, kwani  itasaidia kutokomeza kabisa suala hilo.

Previous
Next Post »