MASTER JAY - "TUZO ZINALENGO LA KUTUDHARILISHA"




MTAYARISHAJI nguli wa muziki wa kizazi kipya nchini, Joachim Kimario 'Master Jay' amesema amekosa imani na Tuzo za Kilimanjaro Music, kwa kuwa zinalengo la kuwadhalilisha baadhi ya wasanii.

Master jay amekosa imani kumetokana na Kamati ya Kilimanjaro Academia ambayo imepewajukumu la kuchagua wasanii kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho kukosa sifa.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Master Jay alisema tatizo linaanzia kwenye kamati hiyo kuchagua wasanii waliokosa sifa na vigezo, huku ikiwa haiko wazi kwa wadau pamoja na wasanii ambao ni washiriki wa tuzo hizo.

Alisema watu waliochaguliwa kwenye kamati hiyo, wamekosa uelewa wa muziki na ndiyo maana wanachagua baadhi ya wasanii waliokosa ubora na kusababisha kupoteza imani ya tuzo hizo kwa jamii nzima.

Mtayarishaji huyo alisema ndiyo maana baadhi ya wasanii wanajitoa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa kuogopa kujidhalilika.

"Sijui ni akina nani wanaounda kamati hiyo kwani imepoteza sifa na ndipo tatizo linapoanzia hapo kila mwaka, kukosa uelewa kwenye kamati hiyo na kutokuwa na uwazi kunachangia malalamiko ya kila siku kwa baadhi ya wadau wa muziki.

"Baadhi ya wasanii wanalalamika sana kuhusu tuzo hizi na ndiyo maana wengi wanajitoa, si kwamba wanajitoa kwa kuogopa kushindana hapana bali kudhailika kwani hizi tuzo sasa zinadhalilisha baadhi ya wasanii," alisema Master Jay

Hata hivyo aliwapongeza kwa kuongeza vipengele vingine kwenye tuzo hizo, ambapo mwaka jana kulikuwa na vipengere 29 na sasa vimeongezwa na kuwa 32.

"Kila mwaka wanapiga hatua 10 mbele na kurudi hatua 30 nyuma, hali ambayo inaonesha hakuna maendeleo yoyote kwenye upande wa tuzo hizo, hivyo wanahitaji marekebisho ili kuwe na usawa na kurudisha imani ya tuzo hizo kwa wasanii," alisema Master Jay.

Kwa upande wake Mratibu wa tuzo hizo kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Angelo Luhala alisema tatizo lipo kwa waandaaji ambao ni Kampuni Bia Tanzania (TBL) kushindwa kutoa elimu ya kutosha kwa wadau wote wa muziki nchini.

Alisema TBL inatakiwa kuelimisha umma kujua kazi ya Kilimanjaro Academia, inavyofanya kazi pamoja na mchakato mzima wa tuzo hizo zinavyokwenda, ili kuepuka ulalamikaji unaojitokeza kwa baadhi ya wadau wa muziki.

"Elimu ikitolewa kwa washiriki pamoja na wadau wa muziki, imani itarudi kwenye tuzo hizo na watajua mchakato mzima unavyofanyika hivyo uwazi wa jambo hilii ndiyo utapunguza malalamiko katika tuzo hizo," alisma Luhala.

Previous
Next Post »