KASHFA YA WABUNGE WA KIKE KUJICHUBUA YAIBUA MJADALA MZITO...!!


KUMBE! Baadhi ya wabunge wa kike ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanatumia vipodozi vinavyochubua ngozi ya juu ya mwili ili wawe na mwonekano mweupe (kama wazungu). 
Kauli hiyo ya kushangaza ilitolewa bungni Mei 9, mwaka huu na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy wakati alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu udhibiti wa dawa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Akizungumza bila kupepesa macho, Mheshimiwa Kessy  alisema kuwa baadhi ya waheshimiwa wa kike ndani ya mjengo wanatumia vipodozi ambavyo vina madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji.
Grace Kiwelu.
MSIKILIZE KWA KINA
“Labda niseme tu TFDA wanapaswa kusimamia kuhakikisha vipodozi vyenye madhara haviingii nchini, watu wengi sana wanaathirika na kupata magonjwa ya kansa ya ngozi.
“Humu ndani (bungeni) wapo waheshimiwa ambao wanatumia vipodozi hivyo ambapo wanapokuja kuumwa serikali inapoteza fedha nyingi kwenda kuwatibia nje ya nchi,” alisema Kessy.
WABUNGE WAMEKASIRIKA?

Habari za ndani zinaweka wazi kwamba, baada ya Mheshimiwa Kessy kuzungumza madai hayo, baadhi ya waheshimiwa hao wameonesha kukasirishwa na kauli hiyo wakisema ililenga kuwachafua.
“Kwa kweli waheshimiwa wangekuwa wanachuja cha kuzungumza, mambo mengine ukiyasikia unapata picha kwamba lengo la msemaji ni kuchafua watu,” aliweka wazi mbunge mmoja alipoongea na gazeti hili huku akigoma jina lake lisiandikwe gazetini.
ALICHOSEMA MTAALAM WA AFYA
Baada ya kauli hiyo ya Mheshimiwa Kessy ambayo ndiyo habari ya mjini kwa sasa, Ijumaa Wikienda lilizungumza na mtaalam wa masuala ya afya ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Alibainisha kuwa tatizo litokanalo na matumizi ya vipodozi vikali ni kubwa sana Bongo na kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele, taifa linazidi kuangamia kwa ugonjwa wa kansa ambayo husababishwa na kujichubua.
“Serikali kupita mamlaka zinazohusika inapaswa kutilia mkazo suala hili na kuhakikisha inathibiti mianya yote ya kuingizia madawa haya ambayo madhara yake ni makubwa kwa taifa, hasa magonjwa ya ngozi kama vile kansa.
“Hii ni hatari kubwa sana, kwa sababu wabunge ambao ndiyo walipaswa kuwa mfano wa kuigwa, badala yake wao wenyewe wanadaiwa kuwa watumiaji wazuri,” alisema mtaalam huyo.
WABUNGE WANENA
Baada ya mtaalam huyo kuweka wazi hali halisi ya madhara ya matumizi ya madaya hayo, Ijumaa Wikienda lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya waheshimiwa wabunge wanawake ambapo kila mmoja alifunguka kivyake:

ZARINA MADABIDA (Viti Maalum CCM)
“Mimi ni Pharmacia (mtayarishaji na mtoaji wa madawa), natambua vema madhara ya hivyo vipodozi. Sina uhakika kama kuna wabunge wanatumia lakini kama wapo basi nawashauri waache mara moja.
“Mimi situmii hata kidogo, si unaniona hata rangi yangu ni maji ya kunde ya asili?!”
GRACE KIWELU  (Viti Maalum- Chadema)
“Mbunge ni mtu mzima huwezi kumzuia. TFDA wanapaswa kufanya kazi yao ya udhibiti, kweli wanaofanya hivyo wapo lakini tunapaswa kuwapa elimu.
“Mimi situmii, kuanzia mikono hadi miguu yangu vinafanana. Hakuna ‘pepsi mirinda’ katika mwili wangu.”
SUZAN LYIMO  (Viti Maalum-Chadema)
“Wabunge wanapaswa wawe mfano, japo hii ni ishu personal (binafsi) lakini ni vema basi wakatazama madhara yake. Vipo vipodozi ambavyo havina madhara na vingine vina madhara.”
CHIKU ABWAO  (Viti Maalum-Chadema)
“Wabunge ni watu wazima, kujichubua ni ishu private (siri). Lakini na yeye Mheshimiwa Kessy kama ameona wabunge wana tatizo hilo anapaswa kuwashauri waache. Mimi natumia vipodozi lakini visivyo na madhara.”
CATHERINE MAGIGE (Viti Maalum-CCM)
“Ni mambo binafsi, kuhusu wanaotumia mimi sina comments (maoni) yoyote. Ningekuwa natumia mimi ungeniona vinavyoniathiri, sijawahi kutumia kabisa jamani.”

ESTER BULAYA (Viti Maalum-CCM)
“Kwanza sikuwepo bungeni siku hiyo mheshimiwa huyo alipotoa hoja yake. Halafu mimi ni mweusi, huwa sipendi kutumia vipodozi vya kuchubua ngozi ili niwe mweupe, napaka mafuta ya kawaida kabisa. Urembo wangu mkubwa mimi upo kwenye nywele.”
ANNA KILANGO  (Same Mashariki-CCM)
“Ha! Haa! Haaa! Mimi situmii jamani, rangi yangu mimi ni natural  (ya asili) hakuna mkorogo hata kidogo, sijui kama wapo wanaotumia.”
SARAH MSAFIRI (Viti Maalum-CCM)
“Hivyo vitu vinahitaji utaalam sana kabla ya kutumia, mimi situmii hivyo sina uzoefu wowote labda uwaulize wanaotumia.”
ZAINABU KAWAWA (Viti Maalum-CCM)
“Ni kauli ya kitawala, siwezi kutolea tamko lakini pia madhara ni ya kitaalam.”

MARY MWANJELWA (Viti Maalum-CCM)
“Baadhi ya waheshimiwa walikwazika lakini kiukweli vipodozi hivyo vina madhara makubwa. TFDA wanapaswa kutoa ufafanuzi juu ya hilo.”
DUKA LATAJWA
Baadhi ya waheshimiwa waliliambia gazeti hili kuwa, waheshimiwa wanaojichubua hutumia vipodozi vyenye ‘kaloraiti’ kutekeleza nia yao na kwamba duka lao kubwa kwa Dar es Salaam lipo Kariakoo kwa jamaa Mkongomani aitwaye Hashim.
Previous
Next Post »