R.I.P BI KIDUDE

HUYO NDIO BI KIDUDE - LEGENDARY.
Marehem Bi Kidude.

 
Mwanamuziki mkongwe katika Taarab Fatuma Bint Mbaraka maarufu kwa jina la Bi Kidude amefariki dunia muda mchache uliopita huko Bububu Zanzibar, sehemu alikokuwa anaugulia kwa kipindi sasa. Mwili wake utahamishiwa kwake Rahaleo na mazishi yatakuwa kesho. Bi Kidude alizaliwa katika kijiji cha Mfagimaringo.

Sifa na jina la Bikidude lilikuwa na kusifika katika jamii yote ya Zanzibari na kuwa kielelezo cha utalii wa visiwa hivyo vya karafuu ambapo hoteli mbalimbali kubwa na zenye hadhi ya juu visiwani humo zimekuwa zikizipa majina migahawa ya hoteli jina la Bikidude, mfano 236 Hurumzi inatumia jina la mgahawa wake jina la 'Kidude'.
Bibi huyu mwenye sauti nzito na inayopenya vyema masikioni mara anapoimba, ni mzaliwa wa Zanzibar lakini asili ya kabila lake ni Mmanyema kutoka Mkoa wa Kigoma, magharibi mwa nchi.
Licha ya kuwa na umri mkubwa (113) , sauti ya Bi Kidude bado ilikuwa ni nzuri na yenye kuvuta hisia, hasa kwa mpenzi wa miondoko ya muziki wa mwambao.

Bi Kidude katika nyimbo zake nyingi alikuwa akiwavutia wengi kutokana na nyimbo zake kubeba ujumbe wa mahaba kama alivyoimba kwenye wimbo wake ’Ya Laiti napenda pasi kifani’ na wakati mwingine mafumbo kwa lugha ya Kiswahili yenye lengo la kufikisha ujumbe kwa watu maalumu kama alivyoimba katika wimbo wake wa ’Muhogo wa Jang’ombe’.

Katika mwaka 1920 tayari alikuwa amekwisha anza kuimba katika vikundi vya sanaa kule kwao, mwaka 1930 alijiunga na Egyptian Musical Club ya Dar es Salaam na kuzunguka miji mingi ya Tanganyika wakati ule , mwaka 1940 alirudi Zanzibar ambako awali alikuwa amekimbia kwa kuwa aliozwa kwa nguvu na mtu aliyemzidi sana umri.

Pia, Oktoba mwaka 2005 alipata Tuzo ya heshima ya msanii mwenye mafanikio makubwa iliyotolewa nchini Uingereza (tuzo ya WOMAX).

Bi Kidude pia liwahi kuimba na Sitti Binti Sadi wakati wa ujana wake, na katika maisha yake Bi Kidude amekwisha zunguka mabara yote akiimba katika majukwaa na wanamuziki maarufu ulimwenguni Mungu Amlaze Pema Peponi Bibi yetu. Amen
Previous
Next Post »