Ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, mjini Dodoma.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameendelea kutupiana vijembe bungeni kwa lugha zilizoelezwa ni za maudhi ikiwemo ya mmoja aliyesema baadhi ya wabunge wana mimba zisizotarajiwa.
Aidha Mbunge wa Kondoa Kusini Juma Nkamia (CCM) wakati anachangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu alimjibu Mbunge wa Mbeya, Joseph Mbilinyi (Chadema) kwamba, “Siongei na mbwa naongea na mwenye mbwa,” kauli iliyozua malalamiko miongoni mwa wabunge. Kuhusu hoja ya mimba zisizotarajiwa, ilitolewa na Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde wakati anachangia hoja ya Waziri Mkuu alisema wapo wabunge wenye mimba zisizotarajiwa. Kauli hiyo ilisababisha Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) kuomba mwongozo wa Spika kuwa kauli ya mbunge huyo ni ya kuudhi na akataka awataje wabunge ambao wana mimba zisizotarajiwa. “Mbunge ametoa kauli ya kuudhi na kiti kimekaa kimya, naomba mwongozo wake mbunge huyu awataje wabunge ambao wana mimba zisizotarajiwa,” alisema Sakaya ambaye hata hivyo aliondoa hoja yake kabla ya Naibu Spika, Ndugai kutolea mwongozo. “Sitarajii kama wabunge mmefikia huko mnataka kuibua mambo ya nguoni, hata hivyo nitatoa mwongozo wangu mchana,” alisema Ndugai. Hata hivyo baadaye Sakaya alimwandikia Naibu Spika kuwa alikuwa ameondoa hoja yake ya kutaka mwongozo. Kuhusu kauli ya Nkamia , alikuwa anataka Bunge lipuuze mikanda ya Mbunge wa Rombo (Chadema) juu ya madai ya kuwepo udini katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akisema ni ya mitaani kwani chuo hicho hakuna hali hiyo. Baada ya Nkamia kusema hivyo, Mbilinyi ‘Sugu’ alipaza sauti na kuhoji na zile za Lwakatare je? “Sugu naomba ukae kimya halafu elewa mie siongei na mbwa naongea na mwenye mbwa,” alisema Nkamia kauli ambayo ililazimu wabunge wa Chadema, Paulin Gekul na Cecilia Paresso na Mbunge wa Kasulu Mjini Mose Machalli kuingilia kati kuomba mwongozo wa Spika. “Mheshimiwa naomba mwongozo wako mbunge wakati anachangia ametumia lugha ya kuudhi kwa kusema haongei na mbwa bali anaongea na mwenye mbwa akimaanisha mbunge ni mbwa na kiti cha Spika ndio wenye mbwa. Mimi sio mbwa naomba mwongozo wako kuhusu lugha hii ya matusi,” alisema Machali. Naibu Spika Job Ndugai alimtaka mbunge huyo kuendelea na mjadala wake na Nkamia akasema “Huo mwongozo ungekuwa umeombwa na mtu makini ningeutilia maanani, lakini mtu mwenyewe anayeomba mwongozo si mtu makini,” hali iliyozua manung’uniko miongoni mwa wabunge. Ndugai baada ya kumruhusu Nkamia alisisitiza kuwa angetoa mwongozo wake mwishoni’ lakini kauli hiyo haikuwafurahisha baadhi ya wabunge na ndipo Gekul alisimama na kueleza namna kiti cha Spika kinavyopendelea wabunge wa CCM hali inayofanya baadhi ya wabunge kuendelea kutumia lugha za matusi. Naibu Spika alitoa fursa kwa Nkamia kufafanua usemi wake huo. Nkamia alimwomba Mbilinyi samahani kwa kutumia lugha hiyo. “Wakati nazungumza hoja yangu Sugu ambaye ni rafiki yangu alikuwa anatoa maneno ya chini chini na mimi kama binadamu niliishiwa uvumilivu ndio maana nikatoa kauli hiyo kuwa sizungumzi na mbwa bali na mwenye mbwa nikimaanisha kuwa sizungumzi na yeye bali nazungumza na baba yake ambacho ni kiti,” alisema Nkamia. Nkamia aliendelea kusema, “Hata hivyo inaonekana maneno yangu yamechukuliwa kuwa ya kuudhi, Sugu ni rafiki yangu na nyimbo zake nazipenda na huwa nanunua CD zake naomba radhi kwa kauli hiyo”.
EmoticonEmoticon