Wasifu wa daktari huyu bingwa utata

DAKTARI bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo (consultant cardiologist), Harun Elmada Nyagori wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, anadaiwa kupachikwa udaktari huo bingwa bila kuwa na sifa zinazostahili, vyanzo kadhaa vya habari vimefichua taarifa hizo.
Vyanzo hivyo vya habari vinadai ya kwamba, hata taarifa zilizopo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro zinathibitisha utata katika wasifu wa kitaaluma wa mtaalamu huyo.
Inadaiwa kwamba kumebainika utata wa taarifa za wasifu wake (CV), kwa mfano, tarehe yake ya kuzaliwa, elimu yake ya sekondari hadi taaluma yake.
Wakati taarifa zake za kiofisi zikidaiwa kuonesha kuwa alisoma elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1993 na kuhitimu mwaka 1998, cheti chake cha kidato cha nne kinaonesha kuwa alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1996 akiwa amepewa cheti cha daraja la nne (division IV) baada ya kufaulu masomo manne alama D, moja alama C na manne yaliyosalia akipata F.
Taarifa zake hazioneshi amepitia mafunzo yoyote ya afya hapa nchini bali zinaonesha amefanya masomo yake ya awali ya utabibu (preparatory foundation course in medicine) kati ya mwaka 1998 na 1999, huko Ukraine katika Chuo Kikuu cha Lugansk State Medical.
Katika mahojiano yake kwa njia ya simu na mwandishi wetu, daktari huyo alikiri kuwa yeye ni daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo lakini akakataa kukiri au kukanusha madai ya hayo dhidi yake, hususan kuhusu elimu yake ya sekondari na jinsi alivyoifikia kiwango hicho cha taaluma ya udaktari.
“Uliza watu wa Wizara ya Afya,” alijibu kwa mkato alipotakiwa kufafanua inakuwaje CV inaonesha alihitimu kidato cha nne 1998 wakati cheti kinaonyesha 1996, kisha akaendelea,
“....una uhakika? Waajiri wangu Wizara ya Afya wanaelewa elimu yangu na nimemaliza lini,” kisha akakata simu akikataa kuzungumzia kwa undani kuhusu madai hayo dhidi yake.
Inadaiwa ya kwamba taarifa hizo rasmi za daktari huyo zilizoko ofisi ya RAS mkoani humo zinaficha mambo muhimu kuhusu mtiririko wa masomo yake pamoja na tarehe yake ya kuzaliwa, hatua ambayo imewafanya baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo kuwa na shaka naye, hususan uhalali wa cheo chake cha kitaaluma cha daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo.
“Ameficha tarehe yake ya kuzaliwa kukwepa kufahamika kwa udanganyifu alioufanya, haonyeshi mafunzo yake ya utabibu (clinical officer) aliyosomea kule Lindi kwani amedanganya,” anadai mmoja wa watu aliosoma naye.
Juhudi za kumpata Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Ritha Lyamuya zilishindikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
Hata hivyo Mganga Mkuu, Wizara ya Afya, Dk. Donan Mbando, alilieleza Raia Mwema kuwa inawawia vigumu kushughulikia suala la serikali kwa kusikia tu mitaani, bali ni pale linapofikishwa kwa maandishi kama malalamiko.
“Kushughulikia suala la serikali lazima tupate complain (malalamiko), hili tumelisikia tu hivi karibuni,” alisema Dk. Mbando alipozungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu, na kuongeza; “Sisi tukishughulikia tunaanzia wapi, wenye malalamiko watuandikie, kama ni mtu au mkoa.”
Kuhusu tuhuma za daktari huyo akiwa mkoani Mbeya, Mganga Mkuu huyo alisema uongozi wa mkoa huo ulipaswa kuieleza wizara kwa maandishi jambo ambalo halikufanyika.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mama Kikuli, naye hakutofautiana na Mganga Mkuu kwa kusisitiza kuwa malalamiko dhidi ya daktari huyo yapelekwe wizarani kwa maandishi.
Inadaiwa ya kuwa, hii sio mara ya kwanza daktari huyo kulalamikiwa na watumishi wenzake wa afya kwani akiwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, alizusha mgogoro mkubwa kiasi cha watumishi wa hospitali hiyo kutishia kugoma iwapo ataendelea kuwapo hospitalini hapo.
Miongoni mwa tuhuma zilizomkabili akiwa Mbeya ni pamoja na za ubakaji dhidi ya mtoto anayedaiwa kuwa ni mmoja wa maofisa usalama mkoani humo, ambapo alisimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Pamoja na tuhuma hizo, watumishi wa sekta ya afya mkoani Mbeya walikuwa wakihoji kanuni zilizotumika kumpandisha cheo mganga mfawidhi huyo kutoka daktari bingwa hadi daktari bingwa mshauri katika kipindi cha miezi miwili tu, kati ya Oktoba na Desemba, mwaka 2009.
Kwa mujibu wa waraka kuhusu miundo ya maendeleo ya utumishi kwa kada zilizo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wa Novemba 2009, sifa za kuingia moja kwa moja katika cheo cha daktari bingwa mshauri ni pamoja na kuwa na shahada ya uzamili ya udaktari au shahada ya uzamivu (PhD) na mafunzo ya ziada (super specialization) katika fani husika ya udaktari kutoka vyuo vikuu vinavyotambuliwa na serikali.
Nyongeza ya sifa hizo ni pamoja na uzoefu kama daktari bingwa usiopungua miaka tisa na mhusika awe amechapisha taarifa mbalimbali za taaluma yake angalau tatu na yeye ndiye mwandishi mkuu katika kipindi cha miaka sita iliyopita, sifa ambazo wanataaluma wa afya mkoani humo walisema daktari mfawidhi huyo hana.
Hoja zilizotolewa na wanataaluma hao wa sekta ya afya nchini zinathibitishwa na taarifa ya daktari huyo, hususan kile kinachodaiwa na vyanzo vya habari kwamba ni udanganyifu kuhusu mtiririko wa elimu yake.
Previous
Next Post »