MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA)
amesema haungi mkono pendekezo la Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya kutaka
kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Mbilinyi
maarufu kama Sugu alisema mapendekezo hayo yametolewa na watu wenye kutaka
kujipendekeza kwa mkuu wa nchi badala ya kufikiria kuutangaza Mkoa wa Mbeya
katika nyanja ya kimataifa.
Alisema Mbeya
ina historia ya kutaka kujitangaza kimataifa na uwanja huo ni fursa pekee ya
kufikia malengo hayo aliyoeleza kuwa yanataka kufifishwa na wateule wa rais.
“Siungi mkono
uwanja kuitwa kwa jina la JK, tunataka jina litakaloasisi uhalisia wa Mbeya nasi
tufahamike kimataifa, kamati ya ushauri ya mkoa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya
mjini, Norman Sigala ilikurupuka kuleta wazo hilo kabla ya kuwasiliana na
wabunge,” alisema.
Alisema hatua
hiyo ya Sigala haiwakilishi mawazo ya wananchi bali inawakilisha mawazo ya mtu
aliyeteuliwa na kwamba wao wakiwa wawakilishi wa Mkoa wa Mbeya kwa ridhaa ya
wananchi hawawezi kukubaliana na suala hilo.
Kauli ya Sugu
iliungwa mkono na wabunge wengine wa Mkoa wa Mbeya, ambapo Mchungaji Lukson
Mwanjale wa Mbeya Vijijini (CCM) alisema anasikitishwa na hatua hiyo ya
kuliwasilisha wazo hilo bila ya kuwashirikisha wabunge.
Alisema
wakati wa kikao cha kamati ya ushauri wabunge wengi hawakuwepo na taarifa hizo
walizisikia baada ya kusoma kwenye vyombo vya habari.
Naibu Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo ambaye pia ni mbunge wa Songwe,
aliomba apewe muda wa kutaka kujua sababu zilizoibua wazo
hilo.
Wazo la
kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe jina la Rais Jakaya Kikwete linazidi kupata
upinzani ambapo awali chama cha NCCR-Mageuzi na kile cha PPT Maendeleo kupitia
kwa viongozi wa Mkoa wa Mbeya vilipinga wazo hilo.
:::TANZANIA
DAIMA:::
EmoticonEmoticon