HII NDIO RIPOTI YA HALI YA AFYA YA ABSALOM KIBANDA

Habari za jioni wakuu,
Muda umekwenda lakini nimeona ni vyema tukashirikishana taarifa fupi tulizopata kutoka Afrika Kusini anakotibiwa Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda kama nilivyoahidi.

1. Tangu walipowasili jana katika hosipitali ya Milpark, Kibanda amekuwa akiendelea na matibabu kwa maana ya kufanyiwa vipimo mbalimbali vikiwamo CT Scan na X Ray hasa kichwani na sehemu nyingine za mwili ambazo zilipata majeraha.

2. Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, jopo la madaktari wenye ujuzi wa aina tofauti, walikuwa akitarajiwa kukutana ili kusoma taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo, ili kutafsiri maana ya matokeo hayo kisha kutoa mwelekeo wa nini kinafuata au aina ya tiba anayopaswa kupata Kibanda.

3. Taarifa nyingine ni kwamba, imebainika kwamba mfupa laini (fizi) uliopo kati ya pua na mdomo ni kama umekatika. Hii natokana na nguvu na nyenzo walizotumia watesaji kumg’oa meno. Kutokana na hali hiyo ana maumivu makali sana kwenye kinywa chake.

4. Pia imebainika kwamba meno kama sita hivi katika kinywa cha Kibanda yamelegea. Haya ni tofauti na yale mawili yaliyong’olewa katika tukio la awali.

5. Kesho Ijumaa Jukwaa la Wahariri litakutana katika mkutano wa wahariri wote ili kujadili hatua zaidi za kuchukua kwa maana mbili; kwanza ni kuhusu matibabu na afya ya Kibanda na pili usalama wa waandishi wa habari kikazi.

6. Uongozi wa Taasisi iitwayo Southern African Investigative Journalism Forum umemtembelea Kibanda katika hosipitali ya Milpark na kueleza masikitiko yake kuhusu yaliyomkuta. Wameahidi kushirikiana na taasisi za kihabari za Tanzania, kuchunguza tukio hilo kwa lengo la kupata majawabu ya nini kilichojiri na sababu za unyama huo.

Tutaendelea kuwaarifu hatua kwa hatua jinsi tutakavyokuwa tukipata taarifa kutoka Afrika Kusini.


--

Neville C. Meena,
Secretary General,
Tanzania Editors Forum - TEF,
Dar es Salaam - Tanzania.
Cell: +255 - 787 - 675555
+255 - 753 - 555556
Previous
Next Post »