Pinda aunda tume kuchunguza matokeo


Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Bushiri, iliyopo Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Mpaji Said (20), akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, akipatiwa matibabu baada ya kudaiwa kunywa sumu ya panya, kutokana na fedheha aliyoipata kwa kutofaulu mtihani wa taifa wa kidato cha nne

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameunda tume itakayochunguza sababu za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa hivi karibuni.
Katika matokeo hayo ambayo yanatajwa kuwa mabovu kuliko yoyote yaliyowahi kutokea katika historia ya Tanzania, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata daraja sifuri.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo alisema kuwa tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki ijayo, ambapo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi.
Lyimo aliwataja wadau wengine watakaohusika katika uchunguzi huo kuwa ni kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa)
“Tume hiyo itahusisha asasi zisizo za kiserikali (NGOs), zinazojishughulisha na masuala ya elimu. Wazazi, walezi na wananchi wote kwa jumla watoe ushirikiano kwa tume, ili ifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Lyimo.
Akizungumzia hatua hiyo ya Pinda, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) alisema wazo hilo ni zuri, lakini kuunda tume bila utendaji hakutakuwa na maana katika elimu nchini.
Alisema kuwa tume nyingi zimeundwa, lakini hakuna tume iliyowahi kuleta mabadiliko na kwamba mara nyingi matokeo ya uchunguzi huwa ni ya kuidhalilisha Serikali.
Msigwa aliongeza kuwa tume hizo hutumia fedha za wananchi na matokeo yake hayatangazwi wala kufanyiwa kazi.
“Serikali ingewaita wadau wa elimu na kuzungumza nao ijue wapi penye matatizo. Halafu maelezo ya wadau hao yajadiliwe bungeni,” alisema Msigwa akiitaka Serikali kuacha kuchanganya ushabiki wa kisiasa pindi zinapowasilishwa hoja muhimu za maendeleo ya taifa na kuongeza:
“Juzi hoja ya Mbatia imetupwa kapuni, hata sisi wabunge tunapeleka hoja nyingi, lakini hazifanyiwi kazi, kwa sababu ya ushabiki.”
Kiongozi wa Jukwaa la Katiba nchini, Profesa Issa Shivji aliwataka Watanzania wasubiri kuona tume hiyo itafanya nini.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, alitaka suala la elimu lisichukuliwe kisiasa, badala yake Serikali itatue kero za elimu, alizosema zinajulikana na kwamba hakuna haja ya kumtafuta mchawi.

 
Previous
Next Post »