Mtoto anayeungua nguo bila kujiona atua Dar


CHRISTINA Mjema (12) kutoka mji mdogo wa Kabuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, ambaye nguo zake zimekuwa zikiungua kwa moto bila ya yeye kuungua amefikishwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maombi.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika Kanisa la House of Prayer, lililopo eneo la Boko Magengeni alipo Christina, ambapo alionekana akiwa mwenye furaha pamoja na mama yake, Calister Massawe.
Akizungumza, Mwanjilisti wa kanisa hilo, Vera Nzowa alisema baada ya kusoma gazeti la Mwananchi Jumamosi toleo la Februari 16 kuhusu mateso aliyokuwa akiyapata binti huyo, uongozi wa kanisa hilo uliamua kuwatuma watumishi wake kwenda kumchukua mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kabuku mjini Handeni.
“Jumatano iliyopita niliongoza wenzangu kwenda katika eneo la Kabuku ili kumtafuta mtoto huyo, ambaye alikuwa katika mateso makubwa,” alisema.
Nzowa alisema kuwa alipofika katika nyumba hiyo alikutana na mama wa mtoto huyo na kumweleza nia ya kanisa hilo, ambapo kutokana na shida alizokuwa akizipata alikubali.
“Tulikwenda polisi kwa ajili ya kutoa taarifa za kuondoka na mama na mtoto huyo nao walikubali kutokana na matatizo, ambayo wamekuwa wakishuhudia yakimpata mtoto huyo,” alisema.
Alisema baada ya kukabidhiwa na polisi na viongozi wa kijiji hicho kwa ajili ya kuondoka naye, walifanya maombi na kumpaka mafuta ya baraka ili kuzuia moto huo usitokee wakati wakisafiri.
Alisema kuwa walisafiri salama hadi katika kanisa hilo na kufanya maombi, ikiwamo mkesha maalumu, ambao ulifanyika usiku wa Alhamisi iliyopita.
“Tangu amefika kanisani hapa tatizo la nguo za mtoto huyo kuwaka moto halijatokea tena, tuna imani hali ile haitajitokeza tena,” alisema Mwinjilisti Nzowa.
Alisema wamebaini kwamba mtoto huyo amekuwa akiteswa kwa nguvu za giza na ushirikina.
“Hapa wamefika mahali pake, tatizo hili haliwezi kujirudia,” alisema.
Ingawa hakusema lini ataruhusiwa kurudi nyumbani Kabuku, lakini alisema kuna mikesha kadhaa imeandaliwa kwa ajili ya kuendelea kumwombea mtoto huyo.
 
Previous
Next Post »