Machinga Mbeya washauriwa kudai haki zao

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo Mbeya, (machinga) wameshauriwa kutumia muda huu kudai haki zao kwa mkurugenzi wa halmshauri ya jiji hilo kwa kuonyeshwa maeneo yao ya kufanyia biashara zao na siyo kusubiri hadi halmashauri inapotaka kuwaondoa katika maeneo yao ndipo na wao waanze kufanya maandamano wakisema wanadai haki kwa nguvu.

Ushauri huo umetolewa na Katibu wa asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Aman The Foundation Of Life (AFL) ya Mbeya, Philimon Mwansasu wakati wa mdahalo uliokuwa umeandaliwa na asasi hiyo kwa vijana wa jijini hapa uliokuwa na mada isemayo ‘wajibu wa Sekta mbalimbali katika kuwaendeleza vijana nchini’ uliofanyika Mbeya.

“Vijana huu ndio muda mwafaka kwenu wafanyabishara kwenda kwa mkurugenzi na kuanza kufanya naye mazungumzo ya kutaka kupata eneo la kufanyia biashara zenu na siyo kusubiri hadi halmashauri ianze kuwaondoa kwa nguvu ndipo mseme mnataka haki kwa kufanya vurugu na maandamano yasiyokuwa na tija kwenu” alisema.

Alisema suluhu ya kupata haki za msingi kwa mtu yoyote ni pale panapofanyika mazungumzo kwa amani zaidi kuliko kufanya mazungumzo wakati kuna vurugu na maaandamano, hivyo ni vyema vijana wakatumia muda wa amani zaidi kudai haki zao kwa viongozi wao na si vinginevyo.

Dk Steven Mwakajumilo ambaye ni mtumishi wa benki kuu tawi la Mbeya, ambaye pia alikuwa miongoni mwa watoa mada mbalimbali katika mdahalo huo, alisema kitendo cha vijana kudai haki zao kwa kutumia maandamano na vurugu ni njia moja wapo ya kutumika na watu wachache kwa maslahi binafsi,hivyo ni vyema vijana wakaepukana na maandamano kama hayo na badala yake watumie zaidi njia ya mazungumzo na viongozi husika kutatua kero zao.

“Niseme tu kwamba kwenu nyinyi vijana, msipende kutumika na watu wachache wanaotaka kujitengenezea majina yao kwa kutumia mianya ya maandamano yenu wakati mkidai haki zenu za msingi, hivyo kupitia jukwaa lenu la vijana mkatumia muda kwa kujadili kero zenu kwa kuwaita wale ambao mnataka kuzungumza nao kwa lengo la kupata ufumbuzi wa jambo lenu lakini si vinginevyo” alisema
Previous
Next Post »