Handeni, Kilindi wazimia kwa njaa


WAKATI wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha njaa ikisababisha baadhi ya wanaume kukimbia familia zao, Wilaya ya Handeni na Kilindi mkoani Tanga, baadhi ya wananchi wameanza kuzimia kwa kukosa chakula kwa muda mrefu huku wengine wakila mizizi.
Habari zilizopatikana wilayani humo zinaeleza kuwa kuna watu 25 walioanguka na kupoteza fahamu kutokana na njaa inayolikabili eneo hilo.
Miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika zaidi kwa njaa, wilayani humo ni pamoja na Kijiji cha Kwandugwa Kata ya Kwandugwa, ambacho inadaiwa kwamba zaidi ya wakazi 25 wa eneo hilo wameanguka kwa nyakati tofauti na kupoteza fahamu kutokana na kudhoofu kwa sababu ya kutokupata mlo wa uhakika.
Hali hiyo inasababisha wananchi hao kuishi kwa kula majani ya porini ya mchunga, makochwe, maembe na wengine kula pumba za mahindi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili juzi lilipotembelea kijijini hapo. Wakazi hao huku wakionekana wachovu kiafya, walisema kwamba wamesikia Serikali ikitangaza kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa njaa nchini, lakini wamedai kwamba kwa hali ilivyo kwao sasa si ajabu wakafa.
“Mimi hivi unavyoniona sijala tangu juzi, ninakula mboga za majani pamoja na familia yangu, kama ni siku kumi, ni kumi hivyo tutapona! tutakufa kwa sababu hatujiwezi, juzi nilifanikiwa kupata kilo moja ya unga ndiyo tuliyopika uji tukala na mboga. Kama hatutapatiwa msaada wa chakula mapema tutakufa,” anasema Mahamudu Athumani (55) mkazi wa Kitongoji cha Chang’ombe

Mbaruku Mahamudu (14) ambaye ni mtoto wa familia hiyo na ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kwandugwa anasema kwamba amelazimika kuacha kwenda shule kutokana na njaa, ambapo anashirikiana na familia yake kutafuta vibarua kwa ajili ya kujikimu.
“Vibarua hapa sasa vimepungua, chakula chetu kikubwa sasa ni mboga, juzi tulikunywa uji pekee, jana tumeshindia kula mboga mchana na usiku na iliyobaki ni hii hapa. Mama hayupo kaenda shambani kutafuta vibarua na baba kaenda kwenye msiba Kwandugwa.
Shule siendi kutokana na njaa,” anasema mwanafunzi huyo akiwa nyumbani kwao Chang’ombe.
Hali kama hiyo ya ukali wa njaa imemkumba pia Mwenyekiti wa Serikali wa kijiji hicho cha Kwandugwa, David Mganga ambaye anasema kwamba yeye bado hajaanguka njaa, lakini wakati wowote kuanzia sasa si ajabu akifikia hapo kutokana na kukosa chakula.
“Hata mimi mwenyewe mwenyekiti kwangu sina hata tone la unga, hapa tuna hali mbaya, tunahitaji msaada wa haraka. Mimi ninaishi kwa kunywa uji na mboga za majani, ilhali nina dhamana ya uongozi naweza kwenda kukopa dukani, wananchi wengine wasio na dhamana hali itakuwaje?” anahoji Mganga na kuongeza kuwa:
“Zaidi ya watu 2,000 hapa kijijini wanalala na njaa, labda kama kuna wanaopata chakula mlo mmoja kwa siku hao ni wachache na ndiyo wenye unafuu wa maisha. Tunaomba Rais Jakaya Kikwete atuokoe kwa kutuletea chakula mapema, vinginevyo ni kweli kabisa watu watakufa,” anasema mwenyekiti huyo.


Previous
Next Post »