Mabaki ya nyumba za marehemu Ernest Mholela zilizobomolewa kabla ya kumzika akiwa hai kutokana na kutuhumiwa kuwa mchawi
KUTOKANA na tukio la watu wawili kuzikwa wakiwa hai hivi karibuni Wilaya ya Mbozi, wazee mkoani Mbeya wameiomba Serikali kuandaa utaratibu wa kutoa ulinzi hasa kwa watu waliopo vijijini.
Wamesema matukio kama hayo yamewajengea woga na kusababisha kuishi kwa hofu hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi zao za kila siku na kushiriki katika shuguli za kijamii vizuri.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa niaba ya wazee hao, Abel Ambakisye alisema tukio hilo limekuwa tishio kwa wazee hasa waishio vijijini na kuleta sifa mbaya ya Mkoa wa Mbeya kuwa ni eneo lenye matukio mabaya.
“Suala hili ni kubwa na baya kwa mkoa wetu, kwani linatutisha sisi wazee kuona watoto na vijana wetu wanatufanyia vitendo vya kinyama kama hiki kilichotokea hivi karibuni cha kuwazika watu wawili wakiwa hai,” alisema.
“Suala hili ni kubwa na baya kwa mkoa wetu, kwani linatutisha sisi wazee kuona watoto na vijana wetu wanatufanyia vitendo vya kinyama kama hiki kilichotokea hivi karibuni cha kuwazika watu wawili wakiwa hai,” alisema.
Aliongeza kuwa “Huu ni unyama hivyo Serikali kupitia polisi inapaswa kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina na kuandaa utaratibu maalumu wa kutupatia ulinzi ili tuweze kuishi kwa amani”.
Alisema huko nyuma Mkoa wa Mbeya ulisikika kwa kuwa na matukio ya uchunaji ngozi watu na upigaji nondo, kitendo ambacho kilisababisha watu wengi kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya kuuogopa mkoa huu.
“Lakini Serikali kupitia polisi walikomesha vitendo hivyo, sasa havipo tena, nguvu hizo sasa zielekezwe katika kupambana na matukio kama haya ya kuwazika watu wakiwa wazima”alisema.
“Tunaomba Serikali ya kijiji pia ihusike katika kuvisaidia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kuhakikisha wazee wanakuwa na ulinzi ili waweze kuishi kwa amani na utulivu na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii bila kubughudhiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa wazee wanatarajia kuonana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani kwa ajili ya kuwasilisha maombi yao na kujadiliana jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo na kuangalia mbinu za kufanya ili kulikomesha.
Ambakisye alisema wananchi wa Mkoa Mbeya wanahitaji kufanya mikakati mbalimbali ya kuleta maendeleo, lakini vitendo kama hivi vinarudisha nyuma jitihada hizo.
“Kwani hata wawezekezaji wataogopa kuja hapa mkoani kwetu kuwekeza, kwa kuwa sifa kubwa inayotangazika mkoani kwetu ni vitendo vya kinyama na hivyo kujenga hofu miongoni mwa wawekezaji,” alisema.
EmoticonEmoticon