Polisi wanne wajeruhiwa kutokana na shambulio la gruneti Mombasa

Baada ya siku kamili ya utulivu katika mji wa Mombasa, polisi walokuwa wanapiga doria kati kati ya mji walishambuliwa na gruneti lililotupwa na vijana wawili walokuwa wanatembea kwa miguu.

Kufuatana na mwandishi wa Sauti ya Amerika Josphate Kioko aliyewasili katika eneo la shambulio ni kwamba mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Mkoa wa Pwani Amros Munyasia, aliwasili mara moja na kuzungumza na waandishi habari.

Bw Munyasia amesema, wameweza kumkamata mmoja kati ya watu wawili wanaoamini walihusika na shambulio hilo na kwamba maafisa wanne wanatibiwa hospitali lakini mmoja kati yao yuko katika hali mahtuti.Shambulio hilo la Jumatano magharibi linatokea baada ya waziri mkuu Riala Odinga kutembelea Mombasa na kusema kwamba anaamini kuna watu walojificha walohusika na ghasia hizo.

"Nia yao ni kuwagawa wakazi wa Mombasa kati ya Wakristo na waislamu kwa lengo la kuzusha mgogoro wa kidini." alisema Raila.

Hata hivyo Raila akizungumza na waandishi habari alikata kueleza ni watu gani anaewadhania kuhusika na ghasia hiyo, akisema tu ghasia kuzuka mara tu baada ya kuuliwa kwa Imam Aboud Rogo inaashiria kulikuwepo na mpango mkubwa zaidi.

Kwa upande wake mbunge wa Mombasa Najib Balala aliyekuwa mshirika wa zamani wa Raila anasema haamini kuna ugomvi wa kidini huko Pwani bali na makundi ya wahuni wanaotumiwa kuzusha ghasia hizo.

 

 

Previous
Next Post »